Mtendaji Mkuu wa TARURA Hamidu Mataka akizungumza kuhusu ujenzi wa madaraja ya mawe 180 ambayo wakala huo itayajenga mwaka huu katika mikoa mbalimbali nchini
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAKALA wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) inatarajia kutumia kiasi cha shilingili Bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja ya mawe kwa mwaka huu wa fedha.
Mtendaji Mkuu wa TARURA, Hamidu Mataka alisema hayo akitoa taarifa kwa wajumbe wa bodi ya Taifa ya mfuko wa barabara inayofanya ziara mkoani Kigoma wakati ikielekea kufanya kikao cha bodi mkoani humo Oktoba 5.
Mataka alisema kuwa ujenzi wa madaraja hayo unalenga katika kuchochea kufungua barabara mpya lakini pia kupunguza gharama kwenye miradi ya madaraja na makalavati ambapo miradi hiyo itaokoa asilimia 50 fedha kama ujenzi huo ungetumia nondo na zege.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA mkoa Kigoma, Edwin Mpinzile alisema kuwa kwa mwaka huu madaraja ya mawe 24 yanatarajia kujengwa mkoani ambapo hadi sasa jumla ya madaraja 109 yamejengwa mkoani humo yaliyogharimu shilingili bilioni 2.4 serikali imeokoa asilimia 79 ya shilingi Bilioni 11.9 ambazo zingetumika kama madaraja hayo yangejengwa kwa nondo na zege.
Akizungumzia ujenzi wa madaraja hayo Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa bodi ya mfuko wa barabara, Octavia Mshiu ameipongeza TARURA kwa ujenzi wa miradi hiyo ambayo imeleta manufaa makubwa katika kufungua barabara mpya hasa maeneo ya uzalishaji.
Mshiu alisema kuwa bodi ya mfuko wa barabara itaendelea kutafuta fedha ili kuona miradi zaidi ya ujenzi wa madaraja ya mawe inajengwa kutokana na uimara na gharama nafuu hivyo kuifanya serikali kuokoa fedha.
Moja ya madaraja ya mawe ambalo limejengwa mkoani Kigoma
0 Comments