Na Matukio Daima Media , Mbarali
KATIKA kuhakikisha wazee wanapata huduma za matibabu ya uhakika Mbunge mteule wa jimbo la Mbarali mkoani Mbeya,Bahati Ndingo amehaidi kuwakatia bima za afya wazee 1000 wasiojiweza wilayani humo.
Ndingo amesema kuwa mara baada ya kuapishwa Bungeni Jijini Dodoma atakamilisha zoezi hilo na kwa kuanzia atalenga zaidi wazee wenye uhitaji mkubwa kwanza kwa kuwashirikisha maafisa maendeleo ya jamii kata katika kuwatambua wazee na kila kata atachukua wazee 50.
Ndingo amesema hayo leo wakati wa maadhimisho ya siku ya wazee duniani ambayo kiwilaya yamefanyika katika kata ya Kongolo Mswiswi Kijiji cha Azimio Mapula.
Amesema kuwa mpango huo wa bima za afya kwa wazee ataanza kutoa bima 1000 kwa kuanzia kwasababu katika wilaya hiyo kuna kata 20 .
"Nitakachofanya ninataka kushirikiana na maafisa maendeleo ya jamii kata kwa kuhakikisha wanaenda kila kata kutambua wazee ambao hawana wategemezi na wenye maisha dunia kwa kuanza nao kwa kuwakatia bima kwa hiyo kila kata watafanya watu 50 ambapo jumla inakuwa 1000 "amesema Mh.Bahati.
Aidha amesema kuwa mwezi Desemba mwaka huu zoezi hilo la ukamilishaji wa bima litakuwa limekamilika kwa Wazee 1000 wasiojiweza wilayani Mbarali kwa kuanzia hatua ya mwanzo.
Kuwa pamoja na changamoto zilizopo za Wazee kumekuwa na jitihada za serikali ambayo inaongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuwa ikijitahidi inahakikisha wanachanganua kuzipatia ufumbuzi changamoto za wazee wa Taifa hili.
Amesema kutokana na sensa iliyopita wilaya ya Mbarali Ina wazee 20,000 pamoja na hayo kwenye sensa iliyopita wamegundua kuna wazee zaidi ya 500 ambao wana hali ya chini ambao wanahitaji msaada na kuwa Sera ya Mh Rais ni kuhakikisha Wazee wanapata matibabu ambapo ni lazima wadau wajitokeze kusaidia.
Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Kanali Denis Mwila ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mbarali amemshukuru Mbunge huyo kwa kuonyesha upendo kwa wazee kwa kuwatia bima za afya wazee 1000 wilayani humo .
"Mhe.Bahati umefanya jambo kubwa Sana kwa wazee hawa bima za afya kwa Wazee 1000 si jambo dogo hili ndugu zangu wengi wetu tunafahamu suala la matibabu kwa Wazee ni muhimu hasa kwa umri waliofikia wanakuwa na maradhi ya mara kwa mara "amesema Kanali Mwila.
0 Comments