Header Ads Widget

ACT WAZALENDO WATOA MAPENDEKEZO KUYUMBA KWA BEI YA ZAO LA KOROSHO

    


 NA HADIJA OMARY,LINDI 

CHAMA cha ACT Wazalendo kanda ya kusini  kimetoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka zitakazosaidia kupandisha bei ya zao la korosho katika minada ya zao hilo inayoendelea hivi sasa 


Kauli ya chama hiko inakuja kufuatia kuwepo kwa bei isiyolidhisha ya korosho katika minada mbali mbali inayoendelea hivi sasa ambapo chama cha ACT kupitia mwenyekiti huyo kimesema changamoto ya Bei kwenye zao la korosho zinahitaji majibu yaliyofanyiwa Utafiti, Masuluhisho ya Kisiasa yatavuruga Zaidi.

 

 

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Oktoba 29 Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Lindi Isihaka Mchinjita  amesema ili wakulima wa zao hilo waweze kupata tija ya kilimo wanachokifanya wanahitaji kupata bei zinazolidhisha sokoni

 


 

Hata hivyo chama hicho kimetoa mapendekezo kadhaa ili kukabiliana na changamoto hiyo ya bei ambapo  mapendekezo hayo ni pamoja na   Serikali kupunguza  utitiri wa kodi, ushuru na tozo kwenye zao la korosho angalau  kwa shilingi 415 ili kumnusuru Mkulima wakati anateseka na bei isiyoridhisha. 

 

Serikali ipeleke haraka muswada wa sheria kupunguza makato ya export levy toka asilimia 15 ya FOB hadi asilimia 9 (single digit) kuhami bei ya soko, Serikali itoe ruzuku ya kufidia soko la korosho ya shilingi 200 kwa kila kilo moja (subsdies) kama ilivyofanya kwenye mahindi huko songea mwaka 2021/2022 wakati soko limeyumba ili kumuokoa mkulima

 

”Serikali imeweka tozo, ushuru na kodi kwa wanunuzi wa korosho zipatazo 12. Eneo hili ni muhimu wananchi wajue kuwa tozo hizi ingawa hazijawekwa moja kwa moja kwa Mkulima inaonekana amewekewa mnunuzi. Lakini ukweli ni kwamba mzigo huu unabebeshwa kwa mkulima wa korosho na ndio hasa hasa inaathiri bei ya korosho mnadani.”

 

Amesema Kwa msimu wa mwaka jana makato na ushuru (indirect charges) katika kila kilo moja ya korosho ilikuwa shilingi 1113. Ambapo kwa Mwaka huu kuna ongezeko la shilingi 180 hivyo kufanya makato yote anayobebeshwa mkulima kwa mgongo wa wanunuzi ni shilingi 1,293.

 

“Mchanganuo wa makato hayo  ni kama ufuatao.Makato ya maendeleo ya zao la orosho (pembejeo) shilingi 110,Ushuru wa watunza maghala shilingi 52,Deni la magunia shilingi 81, Usafirishaji shilingi 300 kutoka shilingi 120 ya mwaka jana (Ongezeko la Sh.180), Ushuru la kusafirisha korosho ghafi nje (Exporty levy) ambayo ni sawa na asilimia 15 ya FOB shilingi 380, ICD shilingi 120, Ushuru wa bandari shilingi 100, Vibali shilingi 10, Kushusha mzigo shilingi 10, Provisional income tax shilingi 70

Tozo ya kupakia mzigo shilingi 10, Makato mengine shilingi 50”

 

 

“Ushuru na makato ya moja kwa moja (direct dharges)

Kipengele hiki kinalalamikiwa na wakulima wa Korosho ambapo jumla tozo zote ni shilingi 311 anayokatwa mkulima moja kwa moja kwa kila kilo moja. Hii inajumuisha tozo ya Amcos na Union, ushuru wa Halmashauri, Bodi ya Korosho TARI, Mfuko wa Elimu, na kuchangia vijiji na tozo ya usafirishaji kwenda ghala kuu. Hivyo kwa korosho iliyouzwa kwa shilingi 2050 mkulima atapata shilingo 1,739. ”

 

 

Mapendekezo mengine ni Serikali itunge haraka sheria ya sekta ya kilimo, ambayo  itasaidia kuthibiti makundi ya viongozi mbalimbali kujipangia tozo wazitakazo kwa mazao ya kilimo, ikiwemo zao la korosho.

 

Serikali iachane na utaratibu wa soko la awali, ambapo Bodi ya korosho kuanzia mwaka jana 2022 ilianzisha utaratibu wa kutoa kibali kwa makampuni maalum kununua korosho kabla ya minada kufunguliwa kwa lengo la kuchochea ubanguaji wa ndani ambapo uchunguzi uliofanywa na chama hicho umebaini kampuni hizo hazibanwi kikanunu  ili kufanya ununuzi uwe ni kwa mujibu wa  uwezo wao

 

Kampuni zitakazopewa vivutio zipewe kibali cha kununua korosho kwa kiwango kinachoshabihiana na uwezo wa viwanda vyao vya kubangua korosho kwa mwaka.

 

Hatua nyingene inayotakiwa kuchukuliwa ni matumizi ya bandari ya Mtwara ambapo kuhusu gharama iliyoongezeka kutokana na kutumia bandari hiyo wito wao ni    Serikali kufidia hii gharama kwa njia ya ruzuku au kuiruhusu kutumika bandari ya Dar es salaam wakati mchakato wa kukamilisha ushoroba wa Mtwara ukiendelea.

 

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo ni kwamba kwa sasa Bandari hiyo ya Mtwara imesinzia kiuchumi, usafirishaji wa korosho unabebwa mabegani mwa mkulima pekee. Inalazimika makasha ya kubebea korosho yaje tupu na hii imeongeza gharama za usafirishaji kwa kila kasha moja ni dola za marekani 1,000 ambayo ni sawa ni shilingi 2,500,000 ambayo ni sawa na shilingi 312 kwa kila kilo moja ya korosho ambapo Gharama hiyo imebebwa na mkulima na imechangia kupunguza bei ya korosho minadani.

 

"Kwa picha ya nje uamuzi huu unaweza kuonekana ni bora na wenye tija, ila kulingana na hali halisi ya uchumi wa Mtwara, na mahitaji ya kibiashara, uamuzi huu umechangia kupunguza bei ya korosho minadani.

Hoja yetu ni kwamba ili bandari ya Mtwara iweze kutumika vizuri lazima kwanza ufungue Mkoa wa Mtwara ili bandari isitumike tu kupitisha korosho bali itumike pia kubeba mizigo mingine toka ushoroba wa Mtwara unaoundwa na Malawi, Zambia, Msumbiji na Visiwa vya Comoro."

 

 

Katika minada iliofanywa vyama vikuu vya ushirika kwa siku tofauti kutoka Mikoa ya  Lindi na Mtwara , TANUC kinachohudimia wakulima wa halmashauri za Tandahimba na Newala katika mnada uliofanyika oktoba 27 ,  katika tani 6,473 zilizouzwa  bei ya juu ilikuwa 2,060 na bei ya chini ni 2,050 , MAMC kinachohudumia wakulima wa halmashauri za Masasi na Mtwara katika mnada uliofanywa oktoba 27 katika tani 12,817 bei ya juu ilikuwa 2,070 na bei ya chini 1,920

 

Chama kikuu cha ushirika LINDI MWAMBAO kinachohudumia wakulima wa halmashauri za matama, Lindi manspaa na kilwa katika mnada uliofanyika jana oktoba 28 katika tani 4,100  bei ya juu ilikuwa 2,075 na bei ya chini 1,900 ,RUNALI kinachohudumia wakulima wa halmashauri za Ruangwa, Nachingwea na Liwale Mkoani lindi uliofanika leo katika Tani zaidi ya 600 zilizouzwa bei ya juu ni 2,190 na bei ya chini ni 2,090.

 

Baadhi ya wakulima wa korosho katika maeneo tofauti akiwemo Chirstophar Mandoga  na Omary Segele  walisema kuwa licha ya kukubali kuuza korosho zao katika minada lakini hawajalishwa na bei kwani bei zinazojitokeza sokoni haziendani na gharama walizofanya katika mashamba yao

 

 

" ni kweli Serikali imetupatia pembejeo lakini haikutoa kwa mipulizo yote hivyo ni vile tumekubali kuuza kwa kuwa hatuna sehemu ya kuzipeleka hizi korosho zetu"

 

Hata hivyo akiongea kwa njia ya simu kaimu mkurugenzi wa bodi ya korosho Tanzania  frances Alfred alisema kuwa kwa sasa bai zinazojitokeza katika minada licha kuwa ni ndogo lakini bado mkulima wa zao hilo apati hasara kwani gharama za uzalishaji wa zao hilo mpaka korosho inapelekwa katika mnada inafikia shilingi 1,450 kwa kilo moja

 

"Gharama hizo zinajumuishwa pamoja na pembejeo zikiwemo lakini ukumbuke pembejeo wamepewa bure na serikali hivyo endapo ukitoa gharama ya pembejeo mkulima anabakiwa na shilingi 850 mpaka 900 hivyo kwa bei zinazojitokeza mnadani bado mkulima hapati hasara " alisema Alfred 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI