Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP, Dodoma
WANANCHI wametakiwa kuchukua hatua dhidi ya silaha zinazozagaa mitaani na kutumika kinyume na taratibu lengo likiwa ni kuweiweka jamii salama.
Mkuu wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania,Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Eva Stesheni ameeleza hayo jijini hapa wakati akitoa mada ya madhara ya uzagaaji wa silaha ndogo na nyepesi kwa jamii wakati wa kikao cha Mtandao wa Polisi wanawake Tanzania na viongozi wa makundi ya wanawake Mkoa wa Dodoma.
Amesema,wameamua kuwatumia wanawake Katika mapambano hayo Kwa kuwa ni Mashujaa wa ulinzi na amani kwenye jamii na kwamba Kila mwanamke akisimama kwenye nafasi yake hakuna silaha yoyote itazagaa mitaani bila utaratibu.
amesema kuwa madhara ya uzagaaji wa silaha ni makubwa kwenye jamii na hivyo ni wajibu wa kila mwanajamii kuwafichua wanaomiliki silaha kinyume cha utaratibu kuzisalimisha.
"Silaha zina madhara yake zikizagaa mitaani wanaotumia silaha hizo tunawaona kila leo na wengine tunawajua lakini na tuna vifua vya kutunza siri,” amesema
Kwa Upande wake Mkuu wa kitengo cha udhibiti na usajili wa silaha Kamishna Msaidizi wa Polisi, Bertha Neema Mlay amesema kuwa katika jitihada hizo watuhumiwa 220 walikamatwa kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria .
Aidha amesema watuhumiwa 17 walikamatwa kwa kumiliki risasi kinyume cha sheria na kusisitiza kuwa juhudi bado zinaendelea.
“Mwaka jana 2022 baada ya mwezi Septemba jumla ya watuhumiwa 220 walikamatwa kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria na watuhumiwa 17 walikamatwa kwa kumiliki risasi kinyume cha sheria,” amesema
Amesema kila mwaka Septemba huwa ni mwezi wa msamaha wa kusalimisha silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria na baada ya Septemba huanza kuwakamata wanaomiliki silaha hizo kinyume cha sheria.
Amesema kuwa zoezi hilo lilitakiwa kukamilika Septemba 30, lakini limeongezewa muda hadi Oktoba 31,mwaka huu .
Amesema kuwa silaha ina faida ikitumika vyema kwa kazi iliyokusudiwa na wakati muafaka ila zikitumika kiholela na kinyume na ilivyokusudiwa inaleta madhara.
Pia ameeleza kuwa sheria ya udhibiti na usajili wa silaha yam waka 2015 na kanuni zake za mwaka 2016 zinaruhusu mtu binafsi, kampuni kumilikishwa silaha, matumizi yaliyoainishwa kwenye sheria hiyo ni kujilinda binafsi, kulinda mazao na kulinda Wanyama, mashindano ya kulenga shabaha.
"Silaha inayomilikiwa kinyume na sheria ni silaha haramu," Amesema Mlay.
Alisema kuwa madhara ya uzagaaji wa silaha ni kuongeza uhalifu migogoro, matishio, vita vya wenyewe kwa wenyewe na kurudisha nyuma maendeleo.
Amebainisha kuwa kuwepo kwa silaha hizo huleta ukatili wa kijinsia, kubaka, kulawiti, kilema cha kudumu, kuzorota kiuchumi.
"Kila ifikapo Novemba mosi wataanza kuwakamatawote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria,"amesisitiza .
Akizungumza kwenye mkutano huo, mmoja wa viongozi wanawake kutoka soko la Sabasaba Anna James,ametaka mabalozi kuwa na utaratibu wa kuwatambua watu wanaoingia kwenye maeneo yao ili kupunguza uhalifu.
“Kuna maeneo ukienda lazima mwenyeji atoe taarifa kwa balozi wa nyumba 10, jambo hilo husaidia kujua pale uharifu unapotokea,” amesema
Na kuongeza“Kama maadili yameharibika hata wanawake wengi wanauawa kwa kutumia silaha.
Pia ametaka kuangaliwa kwa kisu kama silaha hatari kwa Maisha ya binadamu kwani kimekuwa kikitumika kufanya mauaji katika matukio mengi.
0 Comments