Seleman Kwirusha Diwani wa kata ya Kumunyika ambaye ameteuliwa tena kuwa Makamu Mwenyekiti Halmashauri ya mji wa Kasulu
Fadhili Abdallah,Kigoma
BARAZA la madiwani la halmashauri ya mji wa Kasulu limemchagua kwa kauli moja diwani wa kata ya Kumunyika Seleman Kwirusha (pichani) kuwa Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa mara nyingine.
Katika uchaguzi huo uliofanyika baada ya Makamu Mwenyekiti huyo kumaliza muda wake wa mwaka mmoja madarakani kwa mujibu wa kanuni alichaguliwa kwa kupata 18 ya wajumbe wa baraza hilo kati ya wajumbe 19 waliohudhuria.
Akitangaza matokeo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Kasulu,Dolla Kusenge ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo alisema kuwa Makamu Mwenyekiti huyo alipata kura 18 za ndiyo na kura moja ya hapana ambapo wajumbe watatu hawakuhudhuria uchaguzi huo.
Baada ya uchaguzi huo Makamu Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu aliwaomba madiwani wenzake kuungana na kufanya kazi ya kusimamia maendeleo ya halmashauri yao ili kuleta maendeleo kwa watu wake akiwataka watendaji kuzingatia madili na weledi katika utendaji wao.
0 Comments