NA MATUKIO DAIMAAPP, ZANZIBAR
MKE wa Rais wa Zanzibar na Msarifu wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Fondation, Mama Maryam Mwinyi, amesema kampeni ya Afya Bora Maisha bora imelenga kuunga mkono juhudi za serikali katika kufikisha huduma za afya bora kwa wazanzibari wote.
Mama Maryam ambae ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, alieleza hayo wakati akizindua Maryam Mwinyi Walkathon "Afya Bora Maisha Bora" katika viwanja vya Dole Kizimbani.
Alisema anafahamu kuwa kipaumbele cha serikali ni kuimarisha afya ya jamii ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za masafa kwa kuwafuata wananchi walipo.
Aidha alisema ZMBF imezindua program maalum ya ‘Afya Bora Maisha Bora’ inayojumuisha uwepo wa kambi ya matibabu bure kwa wananchi wote wa Zanzibar ili kuunga mkono juhudi hizo.
Mama Maryam alibainisha kuwa ni wazi kuwa kampeni hiyo itasaidia kuwafikia wananchi wengi kufahamu hali yao ya kiafya na kujijengea tabia ya kupima afya zao kwa wakati ili kupunguza mzigo wa gharama za matibabu pale ugonjwa utanapogundulika mapema.
“Tumeona imefika wakati kutanua wigo zaidi kwa kuanzisha program hii maalum ambayo italeta matokeo na tija kubwa kwa wananchi kuwasogezea huduma za afya walipo,” alisema.
Hata hivyo, alisema hatua hiyo ni kuwapatia elimu ya afya, kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na kupata matibabu ambayo yatakwenda mpaka ngazi mbalimbali za rufaa katika hospitali zote nchini.
Alisema program hiyo itaendeshwa kitaalamu zaidi kupitia vigezo na viashiria vitakavyopima na kutoa matokeo yatakayobainika pamoja na lengo mahsusi litakalowawezesha kuandaa chapisho la kitafiti litakalosaidia kupata utatuzi endelevu wa maradhi yanayoambukiza na yasioambukiza.
“Naamini huo utakuwa mchango mkubwa wa taasisi yake katika kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta ya afya,” alibainisha.
Alipongeza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na ZMFB na Afya Check kutoa huduma za matibabu kwa siku tatu hivyo aliwataka wananchi kufika na kutumia fursa hiyo waliyoiandaa mahsusi kupima afya zao ili kuongeza tija na kasi ya maendeleo ya jamii, familia na taifa kwa ujumla.
“Wapi watu ambao wanaogopa kupima hivyo msiogipe kwani unapofahanu afya yako unaweza kugundulika na ukijijua mapema basi unatibiwa kwani wapo watu ambao walikuwa na kensa ambayo wamewahi mapema na wamefanikiwa wamepona kwani mkubike afya yako ndio mtaji wako wa kwanza na sio pesa," alisisitiza.
Hivyo aliwataka madaktari na watoa huduma kuhakikisha zoezi hilo linakwenda kwa ufanisi kwa kusimamia na kuweka utaratibu mzuri wa kuwafikia wananchi wote wanaohitaji huduma watakaofika eneo hilo.
“Najua hakuna kazi nyepesi ila ni wajibu wetu kuihudumia jamii yetu kama maadili ya kazi yetu yanavyotuelekeza,” aliwasisitiza.
Naye Naibu Waziri wa Afya Hassan Khamis Hafidh, alimpongeza Rais Mwinyi kwa dhamira yake njema ya kuinua sekta ya afya kwa kujenga hospitali za wilaya zenye viwango ambazo zitawezesha kutoa huduma kwa wananchi wote Unguja na Pemba ambazo zitaanza kufanya kazi Oktoba 1 mwaka huu.
Aliipongeza Afya Check kushirikiana pamoja kuendesha kambi hizo kwani zinasaidia kujua maradhi mbalimbali ambayo yanawakabili na kupatiwa matibabu bora hivyo aliwasisitiza wananchi kutumia fursa hiyo kupima afya zao na kupenda kufanya mazoezi na kula vyakula ambavyo sio vizuri kwa afya zao ili kupunguza maradhi yasioambukiza ambayo yanachukua nafasi ya kwanza kwa vifo Zanzibar.
Mapema Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Fatma Fungo, alisema taasisi hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali kufikia maisha bora kwa kila Mzanzibari.
Alisema ZMBF imeamua kuongeza program hiyo ambayo ina malengo mahsusi ya kuimarisha afya za wananchi kwa kuendesha kambi za matibabu zitakwenda kila wilaya na mikoa yote ya Zanzibar na zitaendeshwa mara moja katika kila robo mwaka ili kuwafikia wananchi wengi zaidi ikiwemo makundi maalum ya watoto, vijana, wanawake, wanafunzi, wazee pamoja na wananchi wenye mahitaji maalum
Fungo alibainisha kuwa katika kambi hiyo huduma mbalimbali zitatolewa ikiwemo huduma ya uchunguzi wa afya ya msingi kwa maradhi yanayoambukiza na yasioambukiza, vipimo na matibabu ikiwemo chanjo ya uviko 19 na chanjo ya watoto kupitia mradi wanaoshirikiana na Wizara ya Afya.
Alisema hadi kufikia Septemba imeweza kuchanja zaidi ya watu 103,408 kati ya watu laki 122,560 ikiwa ni sawa na asiliminia 88.4.
“Hatua hizi ni kuunga mkono juhudi za kutekeleza sera ya serikali ya kutoa huduma za afya bora, ajenda ya maendeleo endelevu 2030, ajenda ya Afrika ya malengo yaliyowekwa 2063 ambapo huduma hizo zitaiwezesha jamii ya zanzibar kupunguza idadi ya watoto waliodumaa, vifo vinavyotokana na uzazi na vifo vinavyosababishwa na magonjwa yasioambukiza,” alisema.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya Check Dokta Isaac Maro alisema lengo la taasisi hiyo ni kuona watanzania wanapata afya bora.
Alibainisha kwamba ilikuwa ni ndoto yao kuja Zanzibar kushirikiana na watetezi wenzao kuona wanatoa afya bora kwa watanzania na kuzifikia idadi kubwa ya watanzania.
Alisema ndoto ya Rais Mwinyi ni kufikia azma ya kutoka huduma za afya bora kwa wote hivyo wataendelea kushirikiana na taasisi hiyo kuona wanaifikia ndoto hiyo.
Sambamba na hayo alimpongeza Mama Maryam kuonesha dhamira yake njema ya kuona wananchi wanakuwa na afya bora kwa kuwasogezea huduma hizo ambazo zitatolewa bila ya malipo.
Nao wadau waliochangia kampeni hiyo walipongeza Mama Maryam Mwinyi ambae ni mdau mkubwa katika sekta hiyo na maendeleo ya jamii na kuonesha mapenzi yake ya kupenda kushirikiana na wadau mbalimbali na kumhakikishia kuendelea kushirikiana ili kumuunga mkono kupitia kampeni hizo za afya na kuamsha morali ya watu kutambua umuhimu wa kufanya mazoezi katika kuimarisha afya zao.






0 Comments