Na Mwandishi Wetu, Matukio Daima App.
MKUU wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar Es Salaam (ZCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Faustine Mafwele analalamikiwa kufungia jalada namba STK/IR/11978/2022 hali inayoelezwa kuwa inachelewesha kufikishwa mahakamani Wilson Kiguha Chacha ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Wikicha Estate Development Agency na wenzake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii ofisini kwake Wakili wa mlalamikaji Frank Chundu alisema tukio hilo lilitokea Desemba 2022 lakini hadi sasa watuhumiwa hawajafikishwa Mahakamani, licha ya watuhumiwa wote kukamatwa, kuhojiwa na upelelezi kukamilika.
Alisema hayo kufuatia mwenendo wa ushughulikiaji wa jalada hilo la kesi ya jinai ya kuvunja bar ya Big Mountain iliyopo Banana Ukonga usiku nakuiba, kukwama kila wakati katika ofisi yake.
Chundu aliendelea kusema kuwa awali jalada hilo lilikwama ofisini kwake kwa zaidi ya miezi mitatu huku Askari polisi wa kituo cha Stakishari wakizuiwa kukamata watuhumiwa wanaohusika na jalada hilo.
“Baada ya kukwama kwa muda wote huo Waziri wa Mambo ya Ndani Mhandisi Hamad Masauni aliingilia kati hali iliyosababisha jalada hilo liibuliwe na kulirudisha kwa wapelelezi wa kituo cha Polisi Stakishari ili waendelee na upelelezi wakimaliza walirudishe kwa hatua zaidi.
Lakini tangu lirudishwe likiwa limekamilika kulingana na maagizo waliyopewa wapelelezi wa kituo cha Polisi Stakishari yapata miezi miwili jalada hilo haijulikani ni nini kinaendelea hadi sasa na wapelelezi wa kesi hiyo hawajui chochote”. Alisema Chundu.
Taarifa kutoka kwa Ofisa wa ngazi ya juu ndani ya ofisi ya ZCO Mafwele zinadai kuwa faili hilo lilipokelewa na kupewa moja ya maofisa wa ofisi hiyo alipitie na kutoa mapendekezo.
“Jalada hilo lilifika kwetu kutoka katika ofisi ya RCO Ilala, lakini lilipofika hapa halikuorodheshwa kwenye kitabu cha masijala namba tatu (3) kama ilivyo kawaida. Isipokuwa alipewa Ofisa mwenzangu alipitie na kutoa mapendekezo na alifanya hivyo kisha kulirejesha kwa ZCO.” Alisema ofisa huyo.
Alipotafutwa ZCO Faustine Mafwele kutolea ufafanuzi tuhuma hizo alisema ni kweli yupo likizo lakini alikwepa kuzungumzia tuhuma za kufungia jalada na kwenda likizo kwa madai yeye si msemaji wa jeshi la polisi hivyo aulizwe bosi wake.
“Niko likizo na kazi zinaendelea kama kawaida mambo mengine mi si msemaji aulizwe bosi wangu ndio msemaji”. Alisema Mafwele.
Alipoulizwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Jumanne Muliro kuhusiana na tuhuma hizo alisema amepata malalamiko hayo atayafanyia kazi.
“Ndugu mwandishi wewe sio wa kwanza kuulizia jalada hilo, kwa vile malalamiko yamekuwa mengi nakuahidi nitafatilia kujua kinachoendelea ili tujue nini kinakwamisha”. Alisema Kamanda Muliro.
Awali Waziri Masauni alipokea malalamiko hayo ya askari wake huyo kutuhumiwa kukwamisha askari wenzake kufanya upelelezi wa jalada lililokuwa mezani kwao katika kituo hicho kwa maslahi yake binafsi kwa kushirikiana na mtuhumiwa anayetajwa kuwa ni bilionea Wilson Kiguha Chacha na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo.
Waziri Masauni aliwataka wananchi kutoa taarifa pale wanapoona kunaviashiria vya kuminywa kwa haki zao na askari polisi ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao kwa lengo la kukomesha vitendo hivyo.
Hata hivyo Waziri Masauni amewataka askari wote kufanya kazi kwa weledi kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Licha ya Waziri Masauni kuingilia kati na kutoa maelekezo kukamilika kwa jalada hilo na kupelekwa mahakamani mara moja bado ZCO Faustine Mfwele anaonekana kusuasua kwa kutotekeleza maagizo hayo.
Waliokamatwa na kuhojiwa na Polisi ni Godfrey Chacha ,Joseph Nyagare, Michael Julius Chacha, Amosi Chacha, Elizabeth Kiguha, Ramadhani Salehe (Sheta), Amiri Kaswe(White) na Josephat Mlaki ambao ndio wamiliki wa mtambo uliotumika kuvunja.
Wengine ni Ally Mbulu na Jafari Mbulu ambao ni wamiliki wa kampuni ya udalali inayoitwa Mak Auctioneers Company LTD.
0 Comments