Header Ads Widget

RAIS SAMIA ATOA BIL.9 KUSOMESHA MADAKTARI BINGWA NA WABOBEZI.

 


Na Mbaruku Yusuph, Matukio Daima APP Tanga. 


RAIS Samia Suluhu Hassan ameipa Wizara ya Afya Shilingi Bil 9 kwa ajili ya kusomesha madaktari bingwa na madaktari bobezi 300 ambao watakwenda kufanya kazi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa,Taifa na zile za Kanda.  


Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipofanya mahojiano na mwandishi wa Matukio Daima Blog kwenye kongamano la Jamii Mpya lililofanyika Jijini hapa  na kusema ni kweli Wizara hiyo imepokea pesa hizo kwa ajili ya kusomesha Madaktari hao.


Waziri Ummy alisema maamuzi hayo yamekuja baada ya Serikali kufanya tathmini na kubaini uhaba wa

madaktari bingwa na wabobezi na kupelekea kuona umuhimu wa kuwasomesha Madaktari hao ili waweze kuja kuwasaidia Watanzania.


"Juzi tu tulitangaza nafasi za kuajiri madaktari bingwa na wengi hawakuomba kwa hiyo sisi kama serikali tumeamua kusomesha madaktari bingwa na kufanya hivi ndio tunaweza kukabiliana na uhaba wa madaktari hao"Akisema Waziri Ummy. 


Aidha alisema kuwa katika masomo hayo kutakuwa na madaktari bingwa wa upasuaji wa mipufa,Madaktari bingwa wa jumla,Madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani,Madaktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na wanawake,Madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto na madaktari bingwa wa mionzi sambamba na madaktari bingwa wa masikio pua na koo.



Alisema madaktari 100 kati ya hao Madaktari 300 watasomeshwa katika mfumo wa seti ambao utahusu jopo zima la madaktari katika kitengo husika ili kukidhi uhitaji wa ugonjwa husika.


"Kwa mfano Tanzanian tumeanza kupandikiza figo sasa lazima daktari bingwa wa upandikizaji wa Figo apate masomo akiwa na mtu wa kuuguza muuguzi,mtu wa pharmacy dawa labda na mtu wa mionzi hii ni seti maana yake mgonjwa ataonwa na jopo zima la Madaktari bingwa"Alisema Waziri Ummy.


Hata hivyo alisema masomo hayo yataanza mwaka huu wa 2023/2024 na Serikali itafawafadhili Madaktari hao kwenye vyuo vyote vya ndani na hata nje ya Nchi na kuongeza kuwa maombi yamekwisha anza kupokelewa na baada ya majuma matatu maombi yatafungwa.


Kwa upande wake Mratibu wa Jaamii Mpya Taifa Ally Makwiru alisema lengo la kuanzishwa kwa Jamii Mpya ni kumuongezea Rais wafuasi na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali kwa maslahi ya Taifa.


Makwiru alisema kwenye Kongamano hilo kuwa Jamii Mpya ipo mikoa 18 kati ya mikoa 26 Tanzania Bara na wameazimia kumuunga mkono Rais zaidi katika mchakato wa uwekezaji wa mradi mkakati wa Bandari ya Dar es salaam na Kampuni ya Dubai Ports World (DP WORLD).


"Tunamuomba Rais asikate tamaa na yanayozungumzwa na wanasiasa na watu ambao wanaweza kumkatisha tamaa kutokana na kauli wanazozitoa hasa katika swala la bandari"Alisema Makwiru.


Mratibu wa Jamii Mpya Tanga Mwajuma Seleman alisema lengo la Jamii hiyo ni kutaka kutoa elimu zaidi kwa Watanzania juu ya mambo aliyoyafanya Rais katika sekta mbalimbali na miradi ya maendeleo hasa katika maeneo ambayo uwelewa wao umekuwa mdogo.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI