NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi amesema kuwa, Serikali imeshatoa jumla ya milioni 750 katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata ya Uru kusini.
Prof. Ndakidemi ametoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara ndani ya kata hiyo ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake kutembelea kata zilizopo katika Jimbo hilo kuwaeleza yale yaliyofanywa na Serikali pamoja na kusikiliza kero zinazowakabili wananchi.
Alisema kuwa, fedha hizo zimegusa sekta za miundombinu ya barabara, elimu, maji, kilimo na mikopo kwa makundi maalumu.
Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kuwashawishi wakulima wajiandikishe ili wapatiwe mbolea ya ruzuku kwani dirisha limefunguliwa ambapo pia aligawa miche ya kisasa ya migomba na kuahidi kuwaletea miche bora ya kahawa kutoka TaCRI Lyamungo.
Akipokea kero za wananchi hao, moja ya kero iliyoibuka ni ubovu wa Barabara katika Kata ya Uru kaskazini, ikiwepo ile ya kutokuwepo kivuko katika eneo la Ongoma Chini.
Mbunge aliunga juhudi za wananchi kujenga kivuko hicho kwa kuchangia mifuko 50 ya saruji ambapo aliwaambia wananchi kuwa kero ya ubovu wa barabara ataziwasilisha TARURA.
Kero ya maji iliibuliwa ambapo wananchi walilalamika kuwa maji yamekuwa yakikatika mara kwa mara huku wakilalamikia ucheleweshwaji katika zoezi la kuunganishwa maji kwa wateja wapya.
Akijibu kero hizo, mtaalamu kutoka MUWSA, alieleza kuwa wananchi wamekuwa na tabia ya kuhujumu miradi ya maji kwa kukata mabomba na kuisababishia Serikali hasara kubwa.
Alieleza kuwa, katika wananchi 100 wa Uru Kaskazini waliopatiwa namba ya malipo ili walipie na kuunganishiwa maji, ni watu 6 tuu wamelipa.
"Niwaelimishe wananchi kuwa suluhu kubwa ya kupatiwa huduma ni kulipia, na hakuna maji ya bure hivyo ni vyema wale mliotumiwa namba ya kulipia mlipe ili muunganishiwe huduma ya maji safi na salama" alisema
Mbunge alilaani kitendo cha kukatwa mabomba, na kushauri wananchi kushirikiana na MUWSA ili wapatiwe huduma ya maji.
Kero ya kutokuwepo Uwanja wa mpira katika kata iliibuliwa ambapo Mbunge alishauri kuwa wananchi waendelee kukiomba Chama Cha Ushirika kiwapatie eneo kwani yeye hawezi kuingilia mambo ya ushirika ambayo yanalindwa na sheria za nchi.
Kero ya uchakavu katika Shule ya Msingi Ongoma ambapo Mbunge na Diwani waliahidi kuwa watapeleka kero hiyo katika mamlaka husika.
Katika ziara hiyo Mbunge Prof. Ndakidemi akiwa ameongozana na Katibu wa Wazazi Wilaya ya Moshi Vijijini Andrew Mwandu, Diwani wa Kata Mariam Msoka, viongozi wa CCM Kata na Matawi kutoka Uru Kaskazini na Watendaji wa idara mbalimbali kutoka Serikalini walitembelea mradi wa ujenzi wa mabweni (2), madarasa (6) na matundu ya vyoo (13) katika shule ya Sekondari ya Kisarika ambapo Serikali imetoa shilingi milioni 437.
Katika shule hiyo, serikali imeongeza idadi ya wanafunzi watakaoingia kidato cha tano mwaka huu kutoka 60 hadi 304.
Akiwa shuleni hapo, Mkuu wa shule hiyo alimweleza Mbunge kuwa changamoto iliyokumba utekelezaji wa mradi huo ni uwepo wa mvua ambapo umeathiri upelekaji wa vifaa katika eneo la shule.
"Kutokana na mvua, ujenzi ulichelewa kwani hata katapila lililokuwa linasawazisha maeneo ya ujenzi lilididimia kwenye Ardhi na changamoto nyingine kubwa hapo shuleni ni uchakavu wa baadhi ya majengo ya madarasa yaliyojengwa shule ilipoanzishwa na wazazi.
Mwisho...
0 Comments