Na Arodia Peter - Matukio Daima App, Iringa.
Shirika la kujiletea Maendeleo Vijijini (RDO) lenye maskani yake katika Kata ya Mdabulo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa imeendelea kufanya miradi mbalimbali ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi katika maeneo mbalimbali vijijini.
Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Fidelis Felisi Filipatali inasema kwamba jukumu kubwa la RDO ni kuleta maendeleo vijijini kwa kufanya miradi mikuu mitatu.
Filipatali aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na vyuo vya ufundi ambavyo vitasaidia vijana wengi kuondokana na changamoto ya utegemezi wa wazazi na walezi wao.
Ili kukamilisha adhima hiyo, Filipatali anasema mradi huo wa kuwakwamua vijana utajikita zaidi kwenye ufundi uashi, uselemala na nishati jadidifu.
“Ufundi mwingine ni ushonaji, ufumaji, uchomeleaji, uundaji wa vyuma ufugaji, fundi bomba, magari, mitambo, Tehama na utenegezaji bidhaa za ngozi”ilisema taarifa hiyo ya mkurugenzi na kuongeza:
“Changamoto ya upatikaji wa maji ambayo imedumu kwa muda mrefu maeneo ya Mufindi na sehemu zingine ilifanya RDO waje na mpango mbadala wa kutoa huduma hiyo huku watu waishio katika mazingira hatarishi wakiwemo yatima na wazee wakipata huduma hizo bure.”anasema.
Miongoni mwa kata zilizopata huduma hiyo ya maji imezifikia zaidi ya saba katika Wilaya za Mufindi na Kilolo huku zikitajwa kuwa ni Mdabulo, Ihanu, Luhunga, Mpanga Tazara, Makungu, Kisinga na Mtitu.
Aidha Shirika la RDO limeendelea kuigusa jamii kupitia watoto yatima pamoja na watu wanaoishi kwenye mazingira hatarishi wakiwamo wazee pamoja na wasiojiweza.
Kwa mfano, watoto yatima wamekuwa wakipewa misaada mbalimbali ikiwamo ya elimu, chakula na mavazi huku wazee wazee na wasiojiweza wakijengewa nyumba na kupewa baadhi ya mahitaji ya msingi.
Mratibu wa Elimu na masuala ya Ufundi wa RDO, Obadia Ngailo anasema shirika hilo linasaidia kusomesha watoto yatima kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo huku wakigharamia mahitaji yote ya kila mwanafunzi.
Hadi sasa ni zaidi ya yatima 2000 pamoja na waishio kwenye mazingira magumu wanaendelea kunufuika na huduma hiyo ikiwa ni zaidi ya asilimia 85.
Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya RDO Mdabulo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Tanzania, Daniel Mwaisela anasema bodi inaendelea kushirikiana vema na Serikali kwa kuzingatia Sera na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuongeza kuwa wameanza kutoa huduma hiyo nje na Mufindi pamoja na Ngorongoro mkoani Arusha.
Kulingana na huduma na msaada huo mkubwa unaoendelelea kutekelezwa na Shirika la RDO, Sisi kama chombo cha habari cha kijamii, tunaunga mkono juhudi hizo ambazo zinalenga kupunguza lindi kubwa la umasikini si kwa wana Mufindi tu bali nje ya wilaya hiyo.
Aidha MATUKIO DAIMA App tunawasihi wadau wengine wa ndani na nje ya Mkoa wa Iringa kuiga mfano huo wa RDO ili hatimaye jamii zetu ziweze kuondokana na utegemezi ambao unazaa umasikini na kudumaza maendeleo ya mkoa na Taifa kwa ujumla.






0 Comments