Na Fadhili Abdallah,Kigoma
KAMATI ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma imeiagiza serikali wilayani Kigoma kuchunguza na kuchukua hatua kuhusiana na mradi wa ujenzi wa machinjio katika eneo la Machinioni Ujiji mjini Kigoma kutokana na harufu ya ubadhirifu na utekelezaji duni wa mradi huo.
MJUMBE wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM mkoa Kigoma Abdulkadri Mushi alisema hayo akiongoza kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM mkoa Kigoma kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kueleza kuwa hajaridhishwa na taarifa na hali ya utekelezaji wa mradi huo.
Mushi alisema kuwa mradi huo ulioanza mwaka 2018 ukiwa mradi wa miezi 12 lakini hadi sasa haujakamilika na kuanza kutumika huku fedha kiasi cha shilingi 250 kimetumika ambapo alibainisha kuwa hali ya ujenzi inaonyesha kutekelezwa kwa viwango duni hali inayoonyesha kuna dalili ya ubadhirifu wa fedha kwenye mradi huo.
Mjumbe huyo wa Halmashauri kuu ya Taifa alisema kuwa mradi huo una makando kando mengi ikiwemo kuwepo kwa taarifa ya mpango wa ujenzi (BoQ) ukilinganisha na hali halisi ya ujenzi ambapo baadhi ya vitu vilivyowekwa kwenye utekelezaji wa mradi huo havipo kwenye BoQ na muda unaosemwa kuwa utakamilika na hali halisi ya mradi haviendi sambamba.
Awali akitoa taarifa kwa wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM mkoa Kigoma waliotembelea mradi huo Afisa Mifugo wa halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji,Evance alisema kuwa kiachi cha shilingi milioni 265 kimetolewa na UNCDF kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na shilingi milioni 218 zimeshatumika hadi sasa.
Afisa mifugo huyo alisema kuwa baada ya fedha hizo halmashauri ilitenga shilingi milioni 91 na kiasi cha shilingi milioni 30 zilitolewa na kiasi kingine cha shilingi milioni 61 zimetolewa hivi karibuni kuwezesha kukamilisha mradi huo.
Diwani wa kata ya Machinjioni, Himidi Omari amekiri kuingizwa kwenye akaunti ya kata kiasi cha shilingi milioni 61 kuendeleza mradi huo kiasi cha wiki mbili zilizopita na hiyo imetokana na kelele nyingi ambazo amekuwa akipiga kwenye kamati ya fedha na uongozi kwa mradi huo uliopaswa kukamilika mwaka 2020 kushindwa kukamilika hadi leo.







0 Comments