JUMLA ya madereva 257 wa mabasi ya abiria na malori ya mizigo kutoka mkoa wa Iringa na nje ya mkoa huo waliokuwa wamerudi darasani kujifunza upya mafunzo ya udereva katika chuo cha ufundi stadi (VETA) Iringa wamefaulu mtihani wa vitendo katika chuo hicho .
Mratibu wa mafunzo hayo Edmund Enugu akizungumza Leo wakati wa mtihani wa mwisho wa darasani kwa madereva hao chuoni hapo alisema kuwa jumla ya madereva wa mabasi ya abiria 215 na madereva 42 wa malori akiwemo mwanamke mmoja walijiunga na mafunzo ya muda mfupi chuoni hapo kufuatia agizo la serikali la kutaka madereva wote ambao hawana vyeti kurudi vyuo kusoma .
Alisema kuwa mafunzo hayo yalikuwa ni ya wiki mbili na kuwa baada ya mafunzo hayo wamefanya mtihani wa vitendo chini ya askari wa usalama barabarani kwa kujaribiwa uwezo wao wa udereva na wote wamefaulu mtihani huo wa kwanza na jana wameingia katika mtihani wa pili wa darasani ambao wanafunzi wote wamefanya mtihani huo .
Msajili wa chuo cha VETA Baltazar Kinyamaganga alisema serikali imeamua kulifanya Taifa kuwa ni Taifa la viwanda hivyo jukumu la kuandaa mafundi ni la VETA na ofisi yake ya msajili ni usimamizi wa vyuo vya VETA na kuwa vyuo vya VETA Iringa vinaendelea kutekeleza malego ya serikali ya kuona vijana wanakuwa na ujuzi wa ufundi mbali mbali kupitia kozi fupi na ndefu .
Kuwa kozi fupi ni kuanzia wiki mmoja hadi wiki sita na mafunzo ya muda mrefu ni kuanzia mwezi mmoja hadi miezi sita na kuwa kupitia mafunzo hayo mwamko wa jamii kupata mafunzo VETA umekuwa mkubwa zaidi .
Alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika kanda ya nyanda za juu kusini na tayari vyuo katika wilaya ya Iringa na Wanging'ombe unakwenda vizuri wakati Ludewa umekamilika na wilaya ya Kilolo pesa tayari imetolewa .
Kinyamaganga alisema kanda ya Iringa mbali ya chuo cha VETA Iringa kinachofanya kazi vizuri pia kuna vyuo vya Songea, Namtumbo ,Makete na Nyasa navyo vinaendelea vema.
Hivyo aliwataka wahitimu katika mafunzo mbali mbali ndani ya vyuo vya VETA hasa madereva ambao wanatoka nje ya nchini kuendelea kuwa wazalendo la Taifa kwa kueneza sifa nzuri ya nchini badala ya kuanikia siri ama kulitangaza Taifa vibaya nje .
Pia kuepuka kujihusisha na sifa mbaya za wizi na kusafirisha mali za magendo kwani ni sifa mbaya ambazo zinalichafua Taifa na kuharibu taswira nzima ya kazi ya udereva.
Washiriki wa mafunzo hayo Yowel Chatanda na Richard Chongole walisema kuwa mafunzo hayo kwao ni msaada mkubwa kwani kabla ya mafunzo walikuwa wakifanya kazi ya udereva pasipo kuingia darasani na siku zote walijikuta wanapigwa faini za uzembe barabarani kutokana na kutojua sheria za usalama barabarani ambazo sasa wamepatiwa .
Chongolo alisema kuna wakati alipigwa faini na askari wa usalama barabarni baada ya kushindwa kujua kosa lake na hivyo kutakiwa kulipa faini kwa kutojua kosa lake.
" Nilisimamishwa na askari wa usalama barabarani aliniuliza unajua kosa lako nikasema sijui kosa akaniambia kutojua kosa pia ni kosa hivyo natakiwa kulipa faini kwa kosa la kutojua kosa na nililazimika kulipa faini kwa kutojua kosa" alisema
Mkuu wa chuo cha VETA Iringa Pasiens Nyoni alisema kuwa chuo hicho kimeendelea kutoa mafunzo ya udereva na mafunzo mengine mbali mbali kwa ajili ya kuwaandaa vijana kwenda kujitegemea na kuongeza ajira katika fani za ufundi .
Alisema kuwa pamoja na VETA kuendelea kutoa mafunzo ya udereva ila bado ajali zinaendelea kutokea na ndio sababu ya kuja na mafunzo ya muda mfupi kwa madereva kama sehemu ya kuwakumbusha mafunzo waliyoyapata darasani na kupitia mafunzo hayo madereva wameendelea kukumbuka sheria mbali mbali za usalama barabarani.
Nyoni alisema kuwa kupitia mafunzo hayo ya muda mfupi madereva wameendelea kukumbushwa sheria mbali mbali mpya za usalama barabarani yawezekana wakati wakisoma hazikuwepo ama zilikuwepo zimeboreshwa lakini pia ubora wa miundo mbinu wa sasa ni tofauti na wakati huo .
0 Comments