Na Fadhili Abdallah,Kigoma
KATIBU Mkuu wa CCM Daniel Chongolo amesema kuwa changamoto inayojitokeza kwa baadhi ya watu kuonyesha kupinga uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam inatokana na vita ya kiuchumi ambapo baadhi ya nchi hazipendi kuona uwekezaji na uboreshaji huo unafanikiwa.
Chongolo alisema hayo mjini Kigoma akitoa ufafanuzi kuhusu mpango wa serikali kuipa nafasi kampuni ya DP World ya Dubai kufanya ukwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam ambapo uwekezaji huo utaiwezesha bandari hiyo kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza mapato ya nchi.
Katibu huyo Mkuu wa CCM alisema kuwa katika vita ya kiuchumi kuna makundi hayapendi kuona watu wengine wakifanikiwa kama ambavyo kuboreshwa kwa bandari ya Dar esa Salaam kutaiwezesha bandari hiyo kuongeza ukusanyaji mapato kutoka trillion 7.6 kufikia trilioni 26.7 sambamba na kupunguza gharama kwa meli kusubiri kushusha na kupakua shehena katika bandari hiyo.
Pamoja na hilo Chongolo alisema kuwa wameielekeza serikali kutekeleza mpango huo wa uwekezaji kwani una maslahi makubwa kwa watanzania na ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM hivyo CCM italisimamia jambo hilo hadi kuona linafanikiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya uwekezaji mitaji ya umma,Jerry Slaa alisema kuwa mpango wa uwekezaji katika bandari ya Dar es salaam umepata Baraka zote za bunge kupitia taratibu ambazo zimewekwa na bunge hilo ambalo linawakilisha Watanzania.
Slaa alisema kuwa ni lazima Watanzania wawe macho na upotoshaji mkubwa unaofanywa na wapinzani wenye nia ya kurudisha nyuma maendeleo ya serikali ili serikali ionekane haifanyi kitu katika kuwaletea maendeleo watanzania ambapo kupitia uwekezaji huo serikali itongeza mapato ambayo yataenda kugusa maisha ya Watanzania.
0 Comments