NA WILLIUM PAUL, SAME.
WANANCHI wa Jimbo la Same mashariki wilayani Same mkoani Kilimanjaro wameishukuru Serikali kwa kujenga sehemu korofi katika barabara ya Hedaru- Vunta- Miamba kwa kiwango cha zenge hali ambayo itasaidia kufungua uchumi.
Hatua hiyo imekuja mara baada ya Mwenge wa Uhuru kufika na kujionea ujenzi wa barabara hiyo na kuridhishwa na shughuli ya ukarabati wa barabara hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Mallecel alisema kuwa, kujengwa kwa barabara hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi katika kukuza na kuendelea uchumi wao.
Anne alisema kuwa, barabara ambayo ndio njia kuu ya kuunganisha Tarafa za Mamba vunta na Gonja ilikuwa katika hali mbaya kipindi cha nyuma lakini Serikali imesikia kilio cha wananchi na kuikarabati.
"Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasani imeleta maendeleo makubwa katika jimbo letu imemwaga fedha nyingi katika miradi mbalimbali ikiwemo barabara, hospitali, Elimu, Kilimo na nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hasani" alisema Mbunge Anne Kilango.
Aliongeza kuwa "kujengwa kwa hii barabara ni neema kuwa kwetu kwani sasa tunauhakika wa kupita kipindi chote cha mwaka na pia itatusaidia kusafirisha mazao yetu kuyafikisha sokoni kwa haraka na gharama nafuu".
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa barabara vijijini Tarura wilaya ya Same, Mhandisi James Mnene alisema kuwa, barabara hiyo inaunganisha kata sita ambapo inaurefu wa kilomita 42.2.
Mhandisi Mnene alisema kuwa, kwa mwaka huu walipokea milioni 597.5 kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha zenge sehemu za kona hatarishi zilizopo sita zenye urefu wa mita 810 ambapo kazi imefanyika na kazi inayoendelea ni kuweka vibao vya taadhari ya kona pamoja na mifereji.
"Mradi huu mpaka sasa upo katika asilimia 80 na Mkandarasi yupo saiti tunategemea kazi hii kukamilika ndani ya muda mfupi" alisema Mhandisi Mnene.
Kwa upande wake, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023, Abdalah Shaibu Kaim alionyeshwa kuridhishwa na ujenzi wa barabara hiyo na kudai kuwa dhamani ya fedha inaoneka.
Shaibu alisema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyobora na kwa haraka na kuwataka watumishi wa barabara hiyo kuilinda ili iweze kudumu
muda mrefu.
muda mrefu.
Mwisho.
0 Comments