Header Ads Widget

WABUNGE WAIPONGEZA WIZARA, WATAKA ITUMIE MICHEZO KUTANGAZA UTALII, WAISHAURI SERIKALI KUREJESHA VISIWA NA FUKWE WIZARA YA MALIASILI



Na John Mapepele

Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mapinduzi makubwa yanayofanywa hivi sasa chini ya Uongozi wa Waziri Mohamed Mchengerwa na kuitaka wizara hiyo iongezewe bajeti ili iweze kufanya vizuri zaidi katika mwaka wa fedha 2023/24, huku wakipongeza kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutangaza utalii kimataifa.

Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 5, 2023 na wabunge takribani wote wakati wanachangia katika siku ya pili kwenye Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2023/24 iliyowasilishwa bungeni na Mhe. Mohamed Mchengerwa Mei 2, 2023.

Akichangia katika hotuba hiyo, Mbunge wa viti maalum Njombe (CCM) Neema Mgaya ameitaka Serikali kuangalia namna ya kurudisha fukwe na visiwa vyote katika Wizara ya Maliasili na Utalii ili visimamiwe na Bodi ya Utalii nchini ili kuweza kuuza utalii wa nchi kwa pamoja kama inavyofanyika katika nchi nyingi duniani.
Aidha, amesema nchi kama Ushelisheli zimekuwa zikitegemea utalii wa fukwe na bahari pekee ambapo amefafanua kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na fukwe nzuri kuliko nchi nyingi duniani na endapo zitasimamiwa vizuri zitakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi.

Kwa upande mwingine Mhe. Mgaya ameishauri Serikali kuona umuhimu wa kujenga mahoteli kwa ajili ya kuwalaza wageni ambao wameanza kumiminika kufuatia mikakati mizuri iliyowekwa na Wizara na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Filamu ya The Royal Tour.

Naye, Mhe. Benedetha Mshashu ameipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla kwa mikakati ya kukuza na kutangaza utalii na amesema imezaa matunda ambapo ameomba Wizara kuviendeleza visiwa vidogo vidogo 48 vilivyopo katika mkoa wa Kagera ili viweze kuchangia kikamilifu kwenye uchumi.

Akitoa mchango wake Mbunge wa Mafinga (CCM) Mhe. Cosato Chumi amempongeza Waziri Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu, Hassan Abbasi kwa kazi nzuri waliyofanya wakiwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo amewaomba watumie michezo katika kuitangaza Tanzania kimataifa.
Aidha, amewashauri kuanzisha miundombinu mbora kama viwanja vya michezo katika maeneo ya Hifadhi kama taratibu za kiikolojia zinaruhusu kufanya hivyo ili wageni wanapotembelea maeneo hayo waweze kupata burudani ya michezo mbalimbali.

Amepongeza ubunifu wa Wizara wa kutumia shamba la misitu la Sao Hill la Mafinga mkoani Iringa kutumia katika mashindano ya kimataifa ya mbio za magari,huku pia akimshukuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha ili kuboresha uwanja wa ndege wa Iringa.
Mbunge wa Karatu, Mhe. Daniel Awack ameeleza kuwa Wizara imekuwa ikifanya kazi kubwa na nzuri lakini ni muhimu kuwahusisha wananchi katika ngazi zote za uhifadhi ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza badala ya Serikali kwenda peke yake.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS