Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Serikali imetakiwa kuondoa urasimu katika utoaji vibali vya ununuzi wa mazao kwa wafanyabiashara ili waweze kuuza mazao ya wakulima wanakotaka ili kunusuru mazao kuporomoka katika soko.
Hii inakuja kufuatia kuripotiwa kwa taarifa za urasimu huo ambao unasababisha wakulima kushindwa kuuza mazao yao jambo ambalo litawapa hasara kubwa.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Lupembe mkoani Njombe,Mbunge wa jimbo hilo Mhe.Edwin Enosy Swalle akiwa bungeni jijini Dodoma amesema tayari wakulima wake wameanza kuingia hasara kwa kuuza mahindi yao bei ndogo ya shilingi 5000 kwa debe toka shilingi elfu 15 ya awali jambo ambalo bei elekezi inahitajika kutangazwa.
Aidha Mbunge huyo amesema anaamini Waziri wa Kilimo Hussein Bashe anaweza kutatua changamoto za wakulima nchini hivyo anapaswa kuwakomboa wakulima kwa kurahisisha mifumo ya upatikanaji leseni ya uuzaji mazao kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wake waziri wa Kilimo Hussein Bashe amemtoa hofu Mbunge Swalle na kwamba tayari wakala wa Chakula NFRA umeanza kununua mahindi kwa shilingi 600 hadi 700 kwa kilo na kila wilaya vituo vimeanza kufunguliwa.
Sanjari na hilo lakini pia Mbunge Swalle ameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya Kibena Lupembe Madeke kwa kiwango cha Lami kama ambavyo serikali imekuwa ikiahidi mara kwa mara.
Hata hivyo amesema endapo barabara hiyo itajengwa kupitia bajeti ya mwaka wa fedha ujao itasaidia sana wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kuharakisha ukuaji wa uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.









0 Comments