Na Prosper Kulita,Malinyi
Serikali Wilayani Malinyi imeridhia kuanza kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa wakulima kwa mazao ya kimkakati kuanza kutumika msimu huu wa mavuno wa 2023.
Mazao yanayolengwa kuingia katika mfumo huo ni ufuta na korosho ambapo hata hivyo korosho katika msimu uliopita liliuzwa katika mfumo wa stakabadhi ghalani.
Kabla ya maamuzi haya Mkuu wa wilaya ya Malinyi Mheshimiwa Sebastian Waryuba alitoa mwezi mmoja kwa wataalamu wa ushirika na kilimo pamoja na madiwani kutoa elimu kwa wakulima baada ya mvutano mkubwa katika baraza la madiwani juu ya kuanza kutumia mfumo huo.
Katika kikao ambacho kimeketi hivi karibuni na kuongozwa na mkuu wa wilaya ya Malinyi ambae ni mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi imeazimiwa kuanza kutumia mfumo huo kwa vyama vya ushirika vya wakulima tisa vilivyoridhia kuanza mfumo huo.
Akitoa maamuzi hayo Mkuu wa wilaya ya Malinyi Sebastian Waryuba amesema mfumo huo utaanza na vyama hivyo tisa(AMCOS) ambavyo vimeridhia wanachama wake kutumia mfumo huo na kuagiza kutengeneza mfumo wa wazi katika kupokea mazao ya wakulima wa vyama hivyo.
Msimu wa uvunaji wa zao la ufuta unatarajia kuanza hivi karibuni kwa wilaya ya Malinyi ambapo vyama vya msingi vya wakulima tisa vitapokea mazao yao na kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mwezi February mwaka huu madiwani wa Halmashauri ya Malinyi na baadhi ya watalaamu walitembelea wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara kwa ajili ya kujifunza mfumo huo.
Baadhi ya wanachama katika AMCOS tisa wamefurahishwa na maamuzi hayo ya serikali ya wilaya ambapo wamesema elimu waliyopatiwa imesaidia kufahamu faida za mfumo huo.
“Binafsi mimi nimefurahi nadhani sasa itatusaidia kupata pesa ya uhakika ambayo mnunuzi atabanwa na mfumo kutulipa kwa wakati kuliko ilivyouwa awali”amesema Marwa Kashogi kutoka Sofi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI H/W MALINYIP
0 Comments