NA WILLIUM PAUL.
MBUNGE wa Viti maalum kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri ameendelea kuonyesha dhamira yake ya kuwapambania wananchi wa mkoa huo katika kupata majibu ya matatizo ambayo yamekuwa yakiwakabili likiwemo tatizo la ukosefu wa mawasiliano ya simu ya radio.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari Bungeni alisema kuwa, kumekuwepo na tatizo la usikivu wa mawasiliano ya Radio ya Taifa (TBC) baadhi ya maeneo ya mkoa wa Kilimanjaro katika maeneo ya mipakani ambapo wananchi wamekuwa wakilazimika kusikiliza radio za nchi jirani ya Kenya na kupelekea wananchi kukosa habari za ndani ya nchi yao.
Mbunge huyo alisema kuwa jambo hilo amekuwa akiliongea mara kadhaa Bungeni kuwa maeneo ya Rombo vijiji vya Kikelelwa na vilivyopo jirani na mpaka wanalazimika kusikiliza radio za Kenya.
"Rais Dkt Samia Suluhu Hasani nimpongeze kwa kazi kubwa ya kufungua Tanzania katika sekta ya mawasiliano na niiombe Serikali yangu sikivu katika minara hii 758 ifanye jitihada za kupeleka minara katika maeneo ya mipakani ili wananchi wajibunie shirika lao la mawasiliano kwa jinsi linavofavya kazi kuliko kusikiliza radio za wenzetu" alisema Mbunge Zuena.
Zuena alisema kuwa, katika mawasiliano ya simu maeneo hayo ya mipakani mtandao ambao umekuwa ukishika ni wa nchi jirani wa Safari com ambapo umekuwa ukitawala kuliko mitandao ya nyumbani.
Alisema kuwa, walinzi wakubwa wa mipakani ni wananchi wanaoishi jirani na mipaka hivyo kukosekana kwa mawasiliano kwao kunapelekea kukosa kupata taarifa mapema pale ambapo kunakuwa na changamoto yoyote katika maeneo hayo ya mipaka.
Akizungumza pia tatizo la ukosefu wa mawasiliano katika hifadhi ya wanyama ya Mkomazi alisema kuwa, hifadhi hiyo inawanyama wakali, na sasa kumekuwepo na tatizo la wananchi kuporwa mali zao hivyo kukosekana kwa mawasiliano imekuwa ngumu kwao kutoa taarifa ya kuomba msaada.
"Hata askari wa wanyamapori wa maeneo ya hifadhi ya Mkomazi yalituomba kamati kusaidia waweze kupata mawasiliano kwani kunaweza kutokea changamoto yoyote ndani ya hifadhi lakini hawana mawasiliano hivyo niombe minara hii ambayo Rais ameshuhudia utiaji sahihi wake Serikali iangalie maeneo ya hifadhi ili utoaji wa taarifa uwe rahisi" alisema Mbunge Zuena.
Mwisho..
0 Comments