NA WILLIUM PAUL.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amechangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ambapo ameipongeza Wizara ya Elimu na watendaji wote kwa ushiriki wao kufuta Ujinga, Maradhi na Umaskini.
Mbunge Ndakidemi alimshukuru Rais kwa uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya elimu ambapo alijikita katika ubora wa vyuo vikuu vya Tanzania ukilinganisha na vyuo vya Afrika na duniani kwa ujumla.
Mbunge alisema licha ya nchi yetu kuwa na miundombinu bora ya elimu, vyuo vikuu vya Tanzania havina nafasi nzuri barani Afrika ukilinganisha na Afrika Kusini, Kenya na Uganda.
Alisema kuwa viongozi wetu wa vyuo vikuu wamekosa ubunifu kutangaza vyuo vyao pamoja na baadhi ya wasomi wa vyuo vyetu vya Kitanzania kutochapisha tafiti zao kwenye majarida ya kimataifa.
Alieleza athari za kufanya hayo ni nchi kukosa heshima ya kimataifa na Wahadhiri kupoteza umaarufu kwenye jukwaa la wasomi hali ambayo imechangia vyuo kukosa wadau wa Kimataifa kufanya nao kazi za kitafiti.
Mbunge alishauri Wizara ihakikishe Wahadhiri na wanafunzi wote wanaosomea shahada ya pili na ya tatu wanajisajili kwenye google scholar, pamoja na Wahadhiri na watafiti wetu wachapishe kazi zao kwenye majarida ya kimataifa, Vyuo vikuu viwe na sera ya kuweka machapisho, picha za matukio yote mtandaoni katika tovuti za vyuo.
Mwisho.
0 Comments