Moja ya mashine za kushusha na kupakia shehena katika bandari ya Kigoma
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Maboresho makubwa yaliyofanyika katika bandari ya Kigoma kwa kuongeza vifaa vya kisasa vya kupakia na kupakua shehena imeongeza tija ya utendaji wa bandari hiyo hivyo kuchangia kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Mkuu wa bandari za ziwa Tanganyika, Silvestre Mabula alisema hayo Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma na kusema kuwa maboresho hayo yameifanya bandari ya Kigoma kuwa na mafanikio makubwa katika kuongeza usafirishaji wa shehena kwenda na kutoka kwenye nchi za ukanda wa maziwa makuu.
Mabula alisema kuwa kwa zipo mashine tisa za kushusha na kupakua shehena (Folk Lifty, zipo winchi za kuvutwa na gari (Mobile crane) lakini pia zipo trekta zenye winch ambazo zote zinarahisisha usafirishaji wa shehena hivyo inapoharibika mashine moja ipo njia nyinyine ya kuwezesha upakiaji na upakuaji wa shehena kwenye bandari hiyo.
Mkuu huyo wa bandari za ziwa Tanganyika alisema kuwa mwezi bandari ya Kigoma inasafirisha wastani wa tani laki tano kwa mwezi na inakusanya wastani wa shilingi milioni 500 kwa mwezi hivyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha utendaji wa bandari ya Dar es Saalam kwani shehena kubwa inayopitia bandari ya Dar es salaam inaenda nchi ambazo zipo kwenye ziwa Tanganyika.
Julienne Mutabiirwa wakala wa kusafirishaji shehena kutoka kampuni na Shegema Ltd katika bandari ya Kigoma
Pamoja na hivyo Mabula alisema kuwa mwezi Septemba mwaka huu maboresho makubwa ya matengenezo katika bandari ya Kigoma yatafanyika ukiwa ni mradi wa miezi sita mpango ambao utaongeza utendaji wa bandari ya Kigoma na utaondoa kabisa uchelewashaji wa shehena katika bandari hiyo kwenda nchi za ukanda wa maziwa makuu.
Alisema kuwa ziara ya Raisi Samia imeleta mabadiliko makubwa sana kwa utendaji wa bandari hiyo ikiwemo kubadilishwa kwa watendaji ambapo nusu ya watendaji wa bandari hiyo walihamishwa na kuletwa wengine lakini Raisi Samia ametoa maagizo ya maboresho ya bandari nyingine mkoani humo ambazo zitawesha kuongeza tija kubwa kwa utendaji wa mamlaka ya bandari.
Kwa upande wao wasafirishaji wa shehena kupitia Bandari ya Kigoma wameeleza kuridhishwa na utendaji wa sasa wa bandari ya Kigoma huku wakitoa shukrani wa Raisi Samia Suluhu Hassan ambaye wanasema kuwa ziara yake mwishoni mwa mwaka jana mkoani humo imebadilisha na kuboresha kwa kiasi kikubwa utendaji kwenye bandari hiyo.
Mmoja wa wasafirishaji hao Mbaraka Saidi ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Falcon Marine ya Mjini Kigoma alisema kuwa utendaji katika bandari ya Kigoma,Kibirizi na Ujiji umekuwa mzuri kulingana na ratiba ambayo mteja amepangiwa na hakuna usumbufu ambao unajitokeza kama ilivyokuwa awali.
Moja ya mambo ambayo mdau huyo ameeleza ni utekelezaji wa maagizo ya Raisi Samia kuondoa urasimu kwa watendaji wa mamlaka za serikali wanaosimamia uendeshaji wa bandari hizo ambapo kwa sasa malalamiko au changamoto yeyote inafanyiwa kazi kikamilifu na wateja wanafanya shughuli zao kwa uhuru.
Kwa upande wake Wakala wa meli za mizigo katika bandari ya Kigoma kutoka Kampuni ya Shegema, Julienne Mutabiirwa alisema kuwa moja ya mabadiliko makubwa ambayo wanayaona na kufurahia ni ari ya utendaji wa watumishi ambapo msafirishaji anaweza kutumia muda mfupi kushusha au kupakia shehena kwenye meli.
Juliene alisema kuwa kama utendaji utakuwa huu kwa muda mrefu bandari ya Kigoma ambayo ni lango la biashara na shehena kwa nchi za maziwa makuu itakuwa na tija kubwa katika kuimarisha utendaji wa bandari ya Dar es Salaam.
Hata hivyo wasafirishaji hao walisema kuwa bado upatikanaji wa mabehewa ni changamoto kubwa kwao jambo linalofanya baadhi ya shehena kusafirishwa kwa malori jambo ambalo ni gharama kubwa kwa wasafirishaji shehena.
Mwisho.
0 Comments