![]() |
[ |
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
TIMU ya soka ya Airport kutoka kata ya katubuka Manispaa ya Kigoma Ujiji imefanikiwa kuwa bingwa wa mashindano ya kombela polisi jamii linaloandaliwa na ofisi ya Kamanda wa polisi mkoa Kigoma lengo likiwa kutoa elimu na kuhamasisha jamii katika kushiriki kwenye ulinzi na usalama wa maisha yao na mali zao.
Timu ya Airport imefanikiwa kutwaa ubingwa huo katika mchezo wa fainali wa mashindano hayo ya polisi jamii baada ya kuibugiza timu ya Mwandiga kwa mikwaju ya Penati 5 – 4 na hivyo kunyakua zawadi ya Ng’o,mbe mmoja na fedha taslimu shilingi 200,000.
Timu ya Mwandiga iliyoshika nafasi ya pili ya mashindano hayo imepata zawadi ya seti moja ya jezi na pesa taslimu shilingi 150,000 ambapo lawama za viongozi, wachezaji na washabiki wa timu hiyo zimeenda kwa mshambuliaji wa timu hiyo Dotto Samwel ambaye alikosa penati baada ya kuleta mbwembwe wakati akienda kupiga penati hiyo.
Nafasi ya tatu ya mshindi wa mashindano hayo ambayo yalikuwa yanafanyika kwenye uwanja wa Kawawa Ujiji Mjini Kigoma imeenda kwa timu ya Kitongoni ambayo ilipata zawadi ya pesa taslim shilingi 100,000.
Akizungumza wakati wa fainali za mshindano hayo Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Philemon Makungu alisema kuwa mwisho wa mashindano haya ndiyo mwanzo wa maandalizi ya mashindano ya mwakani na kuahidi kuboresha na kuongeza zawadi zaidi.
Kamanda Makungu alisema kuwa mashindano hayo yamepata mafanikio kwa kuwafikia watu wengi na kutoa elimu na hamasa iliyokusudiwa lakini imeweza pia kuendeleza michezo kutoka maeneo mbalimbali ya manispaa ya Kigoma.
Akitoa maelezo kuhusu mashindano Mwenyekiti wa mashindano, Athuman ambaye ni Kamanda wa Polisi wilaya ya Kigoma alisema kuwa jumla ya timu 16 zilishiriki mashindano hayo ambayo yaliendeshwa kwa makundi hadi kufikia mchezo wa fainali.
Akizungumzia ushindi wa timu yake Kapteni wa timu ya Airport, Joram Raphael alisema kuwa kwao wanashukuru kwa ushindi huo wamepambana hadi kufika fainali na kutwaa ubingwa na kwamba mashindano yamewapa nafasi nzuri timu kuweza kushiriki mashindano makubwa zaidi ya hayo na kwamba mashindano yamefanikiwa ikiwa sambamba na kufikisha ujumbe uliokusudiwa.
0 Comments