Wakazi wa Kijiji cha Tungamalenga mkoani Iringa wameendelea kutoa shukrani zao kwa Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) jinsi unavyosaidia Wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi za Kipaumbele kwa kutoa ufadhili wa masomo wa vyuo mbalimbali hapa nchini .
Wakizungumza wananchi hao katika Kijiji cha Tungamalenga kwa nyakati tofauti wamesema Mradi huo umewanufaisha wananchi hao kiuchumi na kielimu kwa ustawi wa watoto wao.
Anjelika Kasimba, ambaye ni Mnufaika wa Mradi wa REGROW amesema REGROW ni miongoni mwa mradi bora ambao mara baada ya kukamilika kwake utaacha alama isiyofutika kwani anaamini Mtoto wake aliyepata ufadhili wa masomo katika Chuo cha Mafunzo ya Wanyamapori Pasiansi mara baada ya kuhitimu masomo yake atajikwamua kiuchumi yeye pamoja na familia yake .
Ameongeza kwamba tokea Mradi huo uanze kugusa maisha ya wananchi wa Tungamalenga yeye pamoja na Wanawake wenzake wamepata hamasa ya kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kurejesha marejesho na pia kuwa Wanufaika wa miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo COCOBA na ufugaji nyuki.
Aneth Kyaulilo ambaye ni Mwezeshaji Jamii wa Mradi wa Regrow amesema Mradi huo umeboresha maisha ya wananchi ambapo katika Kijiji cha Tungamalenga hadi sasa kuna vikundi saba ambavyo vimepewa Mil.48 kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi kupitia Mradi wa REGROW
Ameeleza kuwa Mradi huo wa REGROW umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi na mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa na hii imesaidia vikundi mara baada ya kuundwa vimekuwa vikipewa mafunzo namna ya kuanzisha miradi ya kimkakati kiuchumi
Kwa upande wake Mratibu wa Regrow, Dkt. Aenea Saanya amesema moja ya vigezo vya utekelezaji wa Mradi huo ni kuhakikisha Wananchi wanakuwa wanufaika namba moja katika maeneo yote ambapo Mradi huo unapotekelezwa.
Mradi wa REGROW ulianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kwa kuendeleza Sekta ya Utalii katika Mikoa ya Kusini. Mradi huo unatekelezwa kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Milioni 150 kutoka Benki ya Dunia.









0 Comments