Watu 14 wameripotiwa kufariki dunia Kusini mwa Somalia baada
ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko, shirika la habari la AFP
liliripoti Jumamosi.
Pia mvua hizo zilisababisha uharibifu mkubwa katika miji na
vijiji kadhaa,
Katika mji wa Baardhere jimbo la Jubaland, walifariki watu
watatu wa familia moja, mkuu wa wilaya Mohamed Weli, aliwaambia waandishi wa
habari alipofanya nao mahojiano.
“Wengi wa majeruhi walinaswa kwenye daraja katika mji ambalo
lilisombwa na mafuriko, ilikuwa vigumu sana kuwaokoa watu hawa kwa sababu ya
muda tukio lilitokea na ukosefu wa rasilimali katika mji,” alisema Weli.
Mvua hizo zinaashiria kuanza mapema kwa msimu wa mvua wa
Aprili hadi Juni na zimeleta afueni katika maeneo ya nchi yanayokumbwa na ukame
mbaya zaidi katika miongo minne.
Lakini shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala
ya kibinadamu OCHA lilionya katika taarifa yake ya Jumamosi juu ya hatari ya
kuongezeka kwa magonjwa kama vile kipindupindu, kwani hali ya maisha inaweza
kuzorota.
Mkazi wa Baardhere, Ahmed Omar alisema kumekuwa na mvua
kubwa katika eneo hilo kwa siku tatu mfululizo.
“Mafuriko yaliharibu mji wa Baardhere, nyumba yangu
iliharibiwa na mali zangu nyingi zilisombwa na mafuriko. Namshukuru Mungu
familia yangu ilinusurika, lakini watu watano walikufa katika mtaa wangu
wakiwemo watoto na wanawake,” aliiambia AFP.
Ahmed aliongeza kuwa kwa sasa mji mzima uko chini ya maji na
familia nyingi zilikimbilia maeneo ya juu yaliyoinuka.
Kiongozi wa Jubaland, Ahmed Islam alituma salamu za
rambirambi kwa ndugu wa waliopoteza maisha na kutaka usaidizi wa haraka
upelekwe kwa walioathiriwa na maafa hayo.
Pembe ya Afrika ni moja wapo ya maeneo yaliyo hatarini zaidi
kwa mabadiliko ya hali ya hewa.
Mapema mwezi huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilionya
kuwa karibu watu 100,000 nchini Somalia wanakabiliwa na viwango vya janga la
njaa kutokana na ukame mbaya zaidi kuwahi kukumba eneo hilo katika miongo
minne.
0 Comments