Header Ads Widget

TRC YAAGIZWA KUONGEZA KASI UJENZI WA RELI YA KISASA



Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe, Seleman Kakoso amemtaka Mkandarasi wa reli ya kisasa kwa kipande cha Dar es- salaam-Morogoro na Makutopora kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake ili aweze kukamilisha mradi kwa wakati na muda uliopangwa. 


Mhe, kakoso ameyasema haya wakati kamati ya kudumu ya bunge ya miundombinu ilipokagua reli ya  kisasa ya mwendokasi, kipande cha Dodoma-Makutupora na baadae Makutopora-Morogoro ikiwa ni utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo ya kutembelea na kukagua   utekelezaji wa miradi ya Serikali  iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2022/2023. 


“Tunajua wakati mradi huu wa reli ya kisasa unaanza kulikuwa na changamoto nyingi na ndiyo kwanza miradi ya namna hii ilikuwa inaanza kutekelezwa nchini, lakini sasa Mkandarasi Yapi Merkezi ameshapata uzoefu wa kutosha na Serikali imemuongezea vipande vingine sasa ni jukumu lake kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake ili huu mradi ukamilike haraka kwa mustakabali wa maendeleo ya sekta zingine na Taifa kwa ujumla kwani huu ni mradi wetu wa kimkakati kama Nchi,” amesisitiza Mhe Kakoso.


Akijibu maswali ya Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Mhe Atupele Mwakibete amesema Serikali ya awamu ya sita inaeendelea kuwekeza kwenye ujenzi na maboresho mbalimbali ya Miundombinu ya reli ya kisasa SGR na ile ya kawaida-MGR Nchini ili kuboresha Sekta ya Usafiri na Usafirishaji kwa njia ya reli katika kukuza uchumi.


“Serikali inafanya jitihada za kujenga na kuboresha sekta ya reli nchini na hata kujenga reli mpya za kisasa na kawaida kwa mikoa ambayo hapo awali haikuwa na reli kwa mfumo wa Public-Private partnership, ambapo mpaka sasa mazungumzo na wakandarasi yanaendelea ya ujenzi huo kwa maeneo ya Mtwara-Mbambabay itakayokuwa na urefu wa kilometa 1,000, Tanga –Arusha kilometer 1,028, na Dar es salaam commuter network itakayokuwa na kilometa 1,600,” amesisitiza Mhe Mwakibete.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI