Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF, Bernard Konga amewaondoa hofu waanachama wake kuhusu taarifa zilizozua taharuki kutokana na kuondolewa kwa usajili na huduma kwa watoto walikuwa wanasajiliwa kupitia utaratibu wa Bima ya Afya ya "TOTO AFYA KADI"kwajili ya maboresho.
Taarifa hizo zilizotolewa juzi na ofisi ya mfuko huo zilizokuwa zinasema mfuko huo unafanya maboresho ya utaratibu wa usajili wa huduma kwa watoto waliokuwa wanasajiliwa kupitia utaratibu wa Bima ya Afya ya "TOTO AFYA KADI" Hivyo kwa sasa wazazi au walezi wanashauriwa kuwasajili watoto wao kama wategemezi wao kwenye bima ya afya au kuwasajili kupitia shule wanazo soma.
Akitolea ufafanuzi taarifa hizo jijini hapa Mkurugezi huyo alisema lengo la maboresho hayo ni kuongeza wigo wa wanachama katika mfumo wa bima ya afya kuelekea bima ya afya kwa wote nabkuhakikisha wanachama katika makundi hayo wanajiunga kama familia au kaya au makundi ya wanafunzi kupitia shule wanazosoma.
"Mpango wa TOTO AFYA KADI ulianza rasmi mwaka 2016 baada yakufanyiwa upembuzi na lengo ikiwa ni kuwajumuisha watoto kupitia shule zao ambapo nia ikiwa kufikia kundi kubwa la watoto walio chini ya miaka 18 ambao kitakwimu ni zaidi ya nusu ya wananchi wote ili kufikia azma ya Serikali ya watu wote kuwa bima ya afya,
"Uzoefu huu wa miaka saba wa kulihudumia kundi hili la watoto kupitia utaratibu wa TOTO AFYA KADI umewezesha mfuko kufikia watoto 210,664 walio chini ya miaka 18 na umepelekea mfuko kujifunza mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha,"alisema Konga.
Alisema kati ya maboresho hayo ni pamoja na usajili wa mtoto mmoja mmoja ambayo inachelewesha utekelezaji wa dhana ya bima ya afya ambayo inataka watu kujiunga kwa wingi wao.
"Mfuko umeendelea kushirikiana na shule za Sekondari na msingi ili kusajili wanafunzi na mwitikio unaonesha hii ndio njia sahihi ya kuendelea nayo ili kuhakikisha watoto wengi zaidi wanaosajili na kunufaika na bima ya afya,"alisema.
Akizungumzia maboresho ya utaratibu wa usajili wa hiari kwa kundi hilo la watoto waliochini ya miaka 18 alisema Mzazi au Mlezi anashuriwa kuandikisha mtoto kama mtegemezi kupitia bima zao kwa mwajiri ai vifurushi vya Najali Afya,Wekeza Afya na Timiza Afya pamoja na wazazi wao.
"Vifurushi hivi vinawezesha mtu yeyote mwenye umri wa zaidi ya miaka 18 kujiunga yeye mwenyewe au na mwenza wake au na watoto wake wasiozidi wanne wenye umri vilivyosajiliwa na NHIF kuhudumia wanachama wake,"alisema Konga.
Alieleza kuwa kundi la watoto watakaokosa sifa na vigezo vya kuandikishwa kupitia bima za wazazi kwa mwajiri au vifurushi vya Najali Afya,Wekeza Afya na Timiza Afya wanaweza kuandikishwa kupitia vyuo,Shule au vituo rasmi vya kulelea watoto waishio katika mazingira magumu.
Aidha kwa watoto chini ya miaka 5 ambao watashindwa kuandikishwa kupitia ufafanuzi uliotolewa watumie fursa ya matibabu bila malipo katika vituo vya umma kama ilivyoainishwa kwenye sera ya Taifa ya Afya 2007.
Pia kwa ambao nafasi za wategemezi kwenye bima zao zimejaa kwa maana ya nne za wana watoto zaidi ambao wanahitaji kuwasajili,watashauriwa kuwasajili kupitia vyuo,shule au vituo rasmi vya kulelea watoto waishio katika mazingira magumu vinavyotambulika kisheria huku watoto walio chini ya miaka mitano,fursa ya matibabu bila malipo katika vituo vya umma kama ilivyoainishwa kwenye sera ya Taifa ya afya 2007 inaweza kutumika.
Vilevile kwa wanachama wa TOTO AFYA KADI ambao wapo katika kipindi cha kusubiri miezi mitatu kabla ya kuanza kupata huduma na wale ambao ni wanachama tayari kupitia utaratibu wa TOTO AFYA KADI wataendelea kupata huduma mpaka muda wao uanachama utakapoisha ndipo watashauriwa kujisajili kwa hiari kwenye utaratibu ulioboreshwa.
Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo alieleza faida za usajili wa watoto kupitia shule zao ni kuwezesha utekelezaji wa dhana ya bima ya afya ambayo inataka kusajili watu kwa wingi wao hivyo utaratibu huu utasaidia kufikia kundi kubwa la watoto nchini.
"Utaratibu huu utasaidia kuwapa unafuu wazazi kugharimia matibabu ya watoto wao na kuwa na uhakika wa matibabu kwani utaratibu huu utasaidia dhana ya bima ya afya kujengeka kwa watoto tangu wakiwa wadogo,"alisema.
Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo alieleza manufaa ya kusajili watoto kupitia familia/kaya ni kuwezesha familia nzima kunufaika na si mtoto tu kwani utaratibu huo utawezesha wazazi kupanga mipango ya igharamiaji nafuu wa afya kupitia bima ya afya na hivyo kuepuka gharama za ghafla zinazosababishwa na magonjwa yanayokuja ghafla hiyo itasaidia familia kuepuka umasikini usio wa lazima.
Hata hivyo alieleza utekelezaji wa mpango huo umeanza juzi.
0 Comments