Hatimaye, Jopo la Mawakili wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limefungua kesi ya marejeo katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi Dar es Salaam, kupinga hukumu ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kibaha iliyosababisha bomoa bomoa ya nyumba na kuziacha kaya 266 na wahanga 640 bila mahali pa kuishi.
Kesi hiyo Na.12 ya mwaka 2023 ipo chini ya Jaji Hemed wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi na imetajwa kwa mara ya kwanza jana tarehe 16 Machi 2023.
Katika kesi hiyo, Jopo la mawakili linalowatetea wahanga wa bomoabomoa hiyo, linaiomba mahakama hiyo ione kwamba hukumu iliyotolewa na Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Kibaha ilikuwa ipo kinyume cha misingi ya kisheria na haikuwa na usahihi wala uhalali wowote wa kisheria.
Mbali na Wakili Mwasipu, mawakili wengine wa upande wa utetezi katika kesi hiyo ni Wakili Gaston Shundo Garubindi, Iddi Msawanga na Wakili Mutalemwa Bugeza.
Bomoa bomoa hiyo iliyofanyika Februari pili mwaka huu, ilitokana na hukumu ya Rufaa ya Ardhi Na. 07/2009 iliyotolewa na Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kibaha tarehe 21 Julai 2009 na kutamka kuwa Ndugu Omar Kadri, ndiye mmiliki halali wa eneo la hekta 995.45 lililopo Kata ya Visiga, wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, lililokuwa katika mgogoro baina yake na wajibu maombi ambao ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Zegereni na Baltazar Simeon.
Hukumu hiyo ilifuatiwa na Amri ya Maombi Madogo Na. 176/2022 iliyotolewa na Baraza hilo tarehe 16 Disemba 2022, ambayo ilielekeza kuondolewa kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Zegereni na Baltazar Simeon na watu wote wanaowahusu, katika eneo la mgogoro na kumkabidhi eneo hilo mleta maombi ambaye ni Ndugu Omar Kadri.
Bomoabomoa hiyo iliathiri Mtaa wa Zegereni wa Kata ya Visiga (Kaya 150) na Jonugha wa Kata ya Misugusugu (Kaya 30) yote ya Kibaha Mjini; na Kitongoji cha Matuga cha Kata ya Kawawa, kilicho chini ya Mamlaka ya Mji Mdogo Mlandizi (Kibaha Vijijini) ambapo Kaya 86 zimeathirika.
Akifafanua kwa ufupi baadhi ya hoja zinazojenga msingi wa kesi hiyo ya marejeo, Kiongozi wa Jopo hilo, Wakili Hekima Mwasipu, alisema kwanza hukumu ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kibaha ilitolewa mwaka 2009, lakini Baraza hilo lilipokea Maombi Madogo na likatoa Amri iliyokazia hukumu hiyo mnamo mwezi Disemba 2022, ikiwa ni miaka 13 baadaye tangu hukumu itolewe, hatua ambayo alisema ni kinyume cha sheria kwasababu hukumu husika ilipaswa kutekelezwa ndani ya muda wa miaka 12.
Pili, Wakili Mwasipu amefafanua kuwa walioshitakiwa katika kesi hiyo ya mgogoro wa ardhi walikuwa ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Zegereni na mtu mwingine anayeitwa Baltazar Simeon, lakini katika Hukumu yake, Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kibaha liliamuru kuondolewa pia kwa watu wengine wote wanaowahusu katika eneo la mgogoro, jambo ambalo ni ukiukwaji wa haki kwasababu hao watu wengine hawakuwa sehemu ya kesi hiyo, lakini wameathiriwa na hukumu hiyo bila kupewa haki yao ya asili ya kusikilizwa.
Aidha, aliongeza kuwa kesi hiyo ilianzia Baraza la Ardhi la Kata ya Visiga, lakini hukumu iliyokuja kutolewa imevuka mipaka ya kata hiyo na kuingilia hadi kata nyingine ikiwemo kata ya Kawawa na Kata ya Misugusugu, jambo ambalo pia ni ukiukwaji wa sheria zinazosimamia mabaraza ya ardhi na nyumba kwasababu Baraza la Kata moja halipaswi kufanya maamuzi yanayohusu maeneo ya kata nyingine.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Kibaha Vijijini, Kibaha Mjini na Uongozi wa Wilaya ya Kibaha kinawapongeza mawakili wote wanaowatetea wahanga hao kwa kufungua kesi hiyo ndani ya muda mfupi kwa nia ya kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati kama ilivyoelekezwa.
Chadema inafuatilia kwa karibu mwenendo wa kesi hiyo, huku kikiamini kuwa hatimaye haki itatendeka na itaonekana imetendeka.
Katika hatua nyingine, mdau wa ardhi na aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini (CHADEMA), Edward Kinabo, ametoa wito kwa wananchi wa Kibaha Vijijini na Kibaha Mjini kujiratibu kwa pamoja na kuhudhuria kwa wingi katika Mahakama Kuu Dar es Salaam, Divisheni ya Ardhi ili kufuatilia kwa karibu mwenendo na hatma ya kesi hiyo, kwa kadri ya ratiba zitakazotolewa na mahakama.
Kinabo amesema kesi hiyo inakwenda kutoa shule kubwa na kuwaamsha wananchi wengi wa Kibaha kuweza kujiamini na kuwa na ari ya kupigania haki zao za ardhi pindi zinapoelekea kuvunjwa.
Kwamba anaamini mwenendo na matokeo ya kesi hii, vitasaidia kukomesha vitendo vya dhuluma na ukandamizaji wa haki za ardhi katika wilaya yetu ya Kibaha na maeneo mengine nchini, vitendo ambavyo hufanywa na watu wenye nguvu....hufanywa na miungu watu... dhidi ya wananchi wanyonge wasio na uwezo wa kupigania haki zao kwenye vyombo vya sheria.
*"Jiji la Dar es Salaam limejaa, watu wengi wanakimbilia Mkoa wa Pwani hususan wilaya yetu ya Kibaha kusaka ardhi kwaajili ya uwekezaji, makazi na shughuli nyingine za kibiashara. Leo Kibaha yetu imegeuzwa kuwa gulio la walanguzi na wababe wa ardhi. Ni jukumu letu kuwalinda wananchi hawa wanyonge ili wasigeuzwe kuwa manamba ndani ya ardhi zao walizojaliwa na Mwenyezi Mungu
Tunalazimika kuwalinda kwa kuwapatia msaada wa kisheria kama tunavyofanya sasa, lakini kubwa zaidi, ninaitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi waupe kipaumbele maalum Mkoa wetu wa Pwani kwa kuhakikisha ardhi yote inapimwa kwa haraka na kumilikishwa kwa hati
Mkoa wa Pwani ni Mkoa uliokaa katika jiografia inayofaa kimkakati sana kwa Uwekezaji hasa kwasababu ya reli ya SGR, bandari ya nchi kavu ya Kwala na ukaribu uliopo kati ya Mkoa huu na Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Tanga na pia Bandari ya Bagamoyo inayokusudiwa kujengwa
Kwa hiyo, ninaitaka Wizara ya Ardhi na Mamlaka za Upangaji na Upimaji za ngazi ya Halmashauri, kwamba wasiishie tu kupima maeneo maalum ya wawekezaji, bali wapime pia na mashamba na viwanja vya wananchi na kuhakikisha wanapatiwa hati bila kuchelewa zaidi; vinginevyo ardhi hii ya Pwani inayomezewa mate na matajiri wengi wa ndani na nje ya nchi, itageuka kuwa nuksi na mkosi mkubwa kwa wananchi wetu badala ya kuwa fursa ya kuwakomboa kiuchumi"* alisema Kinabo.
Jana Mawakili wa Utetezi waliiomba Mahakama hiyo itoe wito wa pili kwa washitakiwa Omari Kadri, Mwenyekiti wa Mtaa wa Zegereni pamoja na Baltazar Simeon.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena tarehe 27 mwezi Machi mwaka huu.
Imetolewa Na:
WESTON SINKONDE
Katibu Mwenezi
CHADEMA Jimbo la Kibaha Vijijini.
0 Comments