Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP Tanga.
Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Tanga imesaini mikataba mipya nane ya miradi ya maji na mmoja wa mkandarasi yenye thamani ya zaidi ya Shs Bil 10.
Akizungumza katika ghafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo Meneja wa Ruwasa Mkoa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo alisema miradi hiyo ya maji itatekelezwa katika Wilaya tano Mkoani hapa na kuhudumia zaidi ya wananchi elfu 39 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022.
Mhandisi Lugongo alisema miradi hiyo mipya itakuwa na jumla ya vituo 92 vya kuchotea maji na matanki 9 yenye jumla ya mita za ujazo 1830 na mtandao wa mabomba wenye urefu wa km 168.2 ambayo inategemea kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 1.5.
"Miradi hii itatoa fursa kwa wananchi waliopo Vijijini kuweza kuunganishiwa maji katika majumba yao na kupata huduma hiyo kwa urahisi kuliko ilivyo sasa"Alisema Mhandisi Lugongo.
Aidha alisema lengo la Serikali kupitia mamlaka zake kusaini mikataba hiyo na kuingia makubaliano ya pamoja na wakandarasi ni kuleta ufanisi na tija ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa kufuata kanuni,taratibu na sheria zitakazofuatwa kwa nia ya kukamilisha utekelezaji huo.
Kwa upande Mkuu wa Mkoa Tanga Omary Mgumba ambae alikuwa mgeni rasmi kwenye ghafla hiyo alisema ofisi yake ipo tayari kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo ikamilike kwa wakati na viwango vinavyoendana na thama ya fedha zilizotengwa.
Aidha alisema Serikali haipo tayari kuwavumilia wakandarasi wazembe katika Mkoa wa Tanga na wahakikishe wanafanyakazi kwa weledi na miradi ijengwe kulingana na thamani ya pesa zilizotengwa.
"Serikali ipo pamoja na nyinyi wakandarasi na mtambue pesa za miradi zipo na mtalipwa kwa wakati ikiwa mtaitekeleza kwa mujibu wa mikataba"Alisema Mgumba.
Aidha alisema jitihada za Mh Rais na Serikali yake ya awamu ya sita kuwatumia wazawa kwenye miradi ya maendeleo ni kutengeneza ajira,kukuza uchumi na vipato vya Watanzania kwa ujumla.
Hata hivyo aliwaasa wakandarasi hao walioingia makubaliano ya utekelezaji katika Wilaya hizo tano ambazo ni pamoja na Lushoto,Korogwe, Kilindi, Mkinga na Handeni kuhakikisha wanatoa ajira kwa wananchi katika maeneo hayo.
Naibu Katibu Tawala Mkoa Tanga Newaho Mkisi aliwataka wakandarasi hao kutekeleza miradi hiyo kwa viwango vya ubora uliotakiwa,thamani inayoendana na fedha zilizotengwa sambamba na matakwa ya kimkataba.
0 Comments