Header Ads Widget

ZAIDI YA SH.BIL.45 ZAOKOLEWA BAADA YA KUUNGANISHA MIFUKO MINNE YA KIJAMII NA KUWA PSSSF

Teddy Kilanga, Arusha

Serikali imeokoa zaidi ya sh.bilioni 45 baada ya kuunganisha mifuko minne ya kijamii iliyokuwa ikijitegemea hapo awali na kuwa mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma(PSSSF)


Mifuko hiyo ni PSPF, PPF, LAPF na GEPF ambapo serikali ilifikia uamuzi wa kuiunganisha Agosti Mosi,2018 na kuunda PSSSF.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha wakati akitoa taarifa ya mwenendo wa PSSSF tangu ilipoanzishwa hadi ilipo sasa,Afisa uhusiano wa mfuko huo,James Mlowe alisema kabla ya kuunganishwa kwa mifuko hiyo gharama ya uendeshaji  ilikuwa ni zaidi ya sh.bilioni 128 kwa mwaka.


"Lakini tulipofunga mwaka wa fedha ulioisha 2021/2022 gharama ya uendeshaji wa PSSSF ni sh.bilioni 68 hivyo ni zaidi ya sh.bilioni 47 zimeokolewa na tungekuwa tunaendesha mifuko ile minne ingezidi,"alisema Mlowe.


Aidha aliongeza kuwa kumekuwa na utulivu kutokana na kupunguza malalamiko kwa wateja wake juu ya mafao yao kulinganishwa kwani hapo awali vyama vya wafanyakazi kila mwaka walikuwa wanatembea na mabango ya madai ya usawa.


Mlowe alisema hayo ni baadhi ya mafanikio yaliyopatikana moja kwa moja  ndani ya kipindi cha miaka minne tangu mfuko wa PSSSF ilipoanzishwa.


Pia alisema wakati wanaungana thamani ya mfuko ilikuwa ni trilioni 6.2 kwa mwaka 2018 lakini umefikia trilioni 8.2 na kwa upande wa uwekezaji katika maeneo mbalimbali ni takribani sh.trilioni 7.5 ikiwa kwa yale yanayoonekana sana ni majengo.


"Lakini uwekezaji wa kwenye majengo ni takribani asilimia 15 na tunapowekeza kuna miongozo ya uwekezaji na sera ambapo benki kuu ya Tanzania(BOT) ndio wanaotoa miongozo kila wakati,"alisema Mlowe.


Aidha alisema uwekezaji mkubwa upo kwenye amana za serikali ambazo ni thamani za muda mrefu na mfupi ambapo ni zaidi ya asilimia 60 pia wamewekeza katika benki za biashara takribani sh.bilioni 400 sawa na asilimia tano.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI