Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju ameridhishwa na maendeleo ya Ujenzi wa mabweni ya wanafunzi ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara, Mwanga mkoani Kilimanjaro yanayotarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 104.
Katika ziara yake ya kukagua ujenzi huo, Mpanju amepongeza uongozi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa ujumla kwa namna ambavyo imefanya maendeleo ya kuongeza miundombinu ya Taasisi katika kampasi ya Kisangara ikiwemo madarasa ambayo yamekwishakamilika.
Amesema mabweni hayo yataboresha huduma za malazi kwa wanafunzi na hasa wa kike, haya yote yakifanywa ndani ya kipindi cha miaka miwili tu tangu Taasisi hii ikabidhiwe kampasi hiyo ya kisangara.
Sio kwasababu ya fedha pekee, ila ni kwasababu ya maono, uongozi na usimamizi wenu wa karibu ndio maana tunaona maendeleo haya katika kampasi hii, hongereni sana” alisema Naibu Katibu Mkuu Mpanju.
Madarasa mapya yaliyo jengwa katika kampasi ya kisangara yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 370 yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi mapema mwezi huu wa Disemba 2022 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum Mh. Dorothy Gwajima, na vile vile kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa mabweni unaoendelea ambao umefikia asilimia Hamsini (50) mpaka sasa.
Katika ziara hiyo, Mpanju aliambatana na Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Bi. Vicensia Kagombora wa Wizara hiyo.
0 Comments