Rais Samia Suluhu Hassan (wa tatu kulia) na Waziri wa ujenzi Makame Mbarawa (wa tatu kushoto) wakiweka jiwe la msingi la upanuzi wa bandari ya Kibirizi mjini KigomaRais Samia Suluhu Hassan (katikati) akitembelea na kukagua mradi wa uboreshaji wa bandari ndogo ya Kibirizi mkoani Kigoma
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
RAIS wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali imeamua kufanya upanuzi na maboresho makubwa ya bandari ndogo ya Kibirizi manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma ili kuwezesha biashara baina ya mkoa Kigoma na nchi za ukanda wa maziwa makuu kufanyika kwa tija kubwa.
Akiweka jiwe la msingi la upanuzi wa bandari hiyo mjini Kigoma akiwa kwenye ziara ya kiserikali ya siku nne mkoani Kigoma Rais Samia alisema kuwa serikali inafanya hivyo ili kuurudisha mkoa Kigoma kuwa kwenye hadhi ya kuwa kitovu cha biashara kwa ajili ya nchi za maziwa makuu
"Tunakusudia upanuzi na uboreshaji wa bandari hii ulete tija katika suala la biashara na kukuza uchumi wa mkoa, pia tutaweka meli kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo na abiria hivyo itachochea mkoa kufanya biashara kubwa na chi hizo,”Alisema Rais Samia.
Katika hatua nyingine Rais Samia amewataka wafanyabiashara wa vibanda vya maduka na migahawa katika eneo hilo kukubali kuondoka kwa sasa ili usanifu ufanywe na kufanywa maboresho ya majengo ya utoaji huduma za maduka na migahawa kuwa ya kisasa.
Alisema kuwa maendeleo yanagharama zake hivyo ameomba waondoke kwa utaratibu ambao utawezesha wafanyabiashara hao kurudi kwenye maeneo yao baada ya maboresho ya majengo kufanyika hivyo kutoa agizo kwa Mkuu wa mkoa Kigoma na Halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji kusimamia mchakato huo.
Sambamba na hilo ametoa agizo kwa Waziri wa ujenzi kushughulikia uboreshaji wa barabara inayoingia eneo hilo la bandari kwani barabara iliyopo sasa inapitika kwa shida na haileti tija kwenye mchakato wa kufanya biashara kwa ufanisi.
Awali akisoma taarifa kwa Rais Samia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya bandari (TPA),Plasduce Mbossa alisema kuwa kiasi cha shilingi bilioni 32 zitatumika kwa ajili ya mradi mkubwa wa uboreshaji wa bandari tatu za Kigoma ikiwemo bandari hiyo ya Kibirizi.ambapo ujenzi wake uhusika na ujenzi wa jengo la abiria na gati la kuegesha meli.
alisema kuwa Ujenzi wa bandari hiyo ambayo inahudumia nchi za ukanda wa maziwa makuu za Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo na Burundi ulianza mwaka 2019 na kwa sasa ujenzi huo umefikia asilimia 69 ambapo majengo yaliyo nchi kavu yamefikia hatua ya ukamilishaji ikiwemo majengo ya ofisi na kazi kubwa iliyobaki kwa sasa ni eneo la kwenye maji huku ujenzi wa bandari ya Ujiji ukifikia asilimia 61.








0 Comments