Na Fadhili Abdallah,Matukio DaimaAPP,
Kigoma
SERIKALI mkoani Kigoma imeanza mkakati wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ambao umeripotiwa kuwepo nchini Uganda ambapo tayari mikakarti mbalimbali ya kujikinga na janga hilo imeanza kutekelezwa.
Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma,Dk.Jesca Leba alisema kuwa tayari wameanza kutoa elimu katika maeneo yenye muingiliano mkubwa, kuweka vifaa vya upimaji na watoa huduma ambao watachukua hatua za haraka pindi atakapobainika mgonjwa.
Mganga huyo wa mkoa Kigoma alisema kuwa wameanza kutoa elimu kwa wahudumu wa afya kwa ngazi ya jamii ambao ndiyo wanaishi na watu kwenye mitaa lakini pia wametenga maeneo ambayo iwapo mgongwa atabainika atapelekwa kwa ajili ya hatua za awali za matibabu, kuwepo kwa magari maalum ya kusafirisha wagonjwa watakaobainika katika maeneo mbalimbali ya mkoa.
Dk.Leba alisema kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa ambaye ameripotiwa mkoani humo lakini hatua za tahadhari zimechukuliwa na mkoa Kigoma ukitajwa kuwa moja ya mikoa mitano ambayo ina nafasi kubwa ya watu kutoka nje ya nchi wanaweza kuingia na kuingiza nchini ugonjwa huo.
Mwenyekiti wa Umoja wa wamiliki wa maboti mkoa Kigoma (UWAMAKI),Kashindi Adam alisema kuwa serikali inapaswa kufanya juhudi kubwa kuhakikisha elimu inatolewa kwa ukubwa wake ili watu wengi waweze kujua hasa kwenye sekta ya usafirishaji kutokan na mwingiliano mkubwa wa watu ambao wanao.
Alisema kuwa boti zao zinasafiri kwenda nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Burundi na Zambia lakini mkoa Kigoma uko karibu na Uganda hivyo kwao tahadhari ya hali ya juu inapaswa kutolewa.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa wasafirishaji wa maboti (UWAKI) mkoa Kigoma, Ibrahim Sendwe alisema kuwa idara ya afya inapaswa iimarishe huduma za upimaji kwenye bandari ndogo ya Kibirizi mkoani Kigoma kwani ni hatari sana kutokana na mwingiliano mkubwa wa wageni wanaoingia na kutoka kupitia bandari hiyo.






0 Comments