Header Ads Widget

WANANCHI WAHOFIA UHAI WA MAISHA YAO KUTOKANA NA TEMBO.

 



NA WILLIUM PAUL, SAME.


WANANCHI wa Kitongoji cha Nadururu kijiji cha Muheza kata ya Maore wilayani Same mkoani Kilimanjaro wapatao zaidi ya 1000 wanaishi mashakani  baada ya wanyama Tembo kuvamia katika Kitongoji hicho na kuuwa mwananchi mmoja aitwae Zuhura Mapande (35).



Wakieleza kwa uchungu huku wakitokwa  na machozi kwa Mbunge wa jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango Malecela alipofika kuwapa pole wananchi hao wamedai  kuwa kwa sasa wanaishi kwa mashaka kutokana na Tembo hao kufika katika maeneo yao ya makazi usiku na mchana.




Emmanuel Elieneza alisema kuwa, wanyama hao wamekuwa wakiharibu mazao ya wananchi na kupelekea wananchi kukumbwa  na baa la njaa.



Akielezea mauaji ya Zuhura alisema kuwa, mnamo Agosti 17 majira ya saa mbili asubuhi marehemu huyo alitoka kwenda kutafuta mboga aina ya mchicha  kwa lengo la kuwapikia  watoto chakula ili waende kuchunga  Mifugo.




"Wakati akiwa njiani kurudi nyumbani ndipo alipokutana na kundi kubwa la Tembo ambapo Tembo mmoja aliyekuwa na mtoto alianza  kumshambulia na kumchanachana vipande vipande wananchi tuliokuwa jirani na eneo hilo tulijaribu kumsaidia lakini ilishindikana" alisema Elieneza.



Kuuwawa  kwa Zuhura kunafanya idadi ya wananchi wa Kitongoji hicho waliouwawa na Tembo kwa mwezi huu pekee kufikia wawili na majeruhi mmoja hali ambayo inapelekea  usalama wa maisha yao kuwa mashakani.




Naye Lun'gwa Abdalla alisema kuwa,  marehemu huyo ameacha watoto sita akiwamo mtoto wa miezi tisa huku baba mzazi wa watoto hao akiwa ameikimbia familia baada ya kuona kila alichokuwa akilima havuni kutokana na mazao kuharibiwa  na Tembo na kuiomba Serikali kuwasaidia watoto hao ambao kwa sasa hawajui hatima yao.



"Huyu marehemu yeye ndio alikuwa baba wa familia alikuwa akiangaika kufanya vibarua katika maeneo mbalimbali ili watoto wake wapate riziki sasa ameuwawa  na Tembo hatujui hatima ya watoto ambao walikuwa wakitegemea mama yao atoke ndipo wale chakula" alisema Abdalla.




Wananchi hao walimuomba Mbunge kuiomba Serikali iweze kuwaangalia kwani hawana pakwenda na wameishi  katika Kitongoji hicho tangu mwaka 1950 huku pia wakisema kuwa hata watoto wao wanaogopa kwenda shule kutokana na kuhofia  maisha yao.



Akitoa salama za pole, Mbunge Anne Kilango Malecela alisema kuwa, tatizo la wananchi kuuwawa na Tembo nchini limekuwa tatizo kubwa na Kitongoji cha Nadururu kwa sasa sio mahali salama kwa wananchi. 




Anne alisema kuwa,  Marehemu  huyo ameuwawa kikatili na Tembo kwa kuchanwachanwa vipande vipande hali ambayo imeleta hofu kubwa kwa wananchi wa jimbo la Same Mashariki.



Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kufika katika Kitongoji hicho na kujenga kituo kwa ajili ya kuzuia Tembo wasiwauwe wananchi kama vinavyojengwa katika wilaya ya Mwanga.




"Nimeshuhudia kule Mwanga Serikali imeanza kujenga kituo kwa ajili ya kuzuia Tembo wasiwauwe wananchi sasa na huku Nadururu nao wanahitaji kituo kwani kwa sasa maisha yao yapo hatarini natambua Serikali ya awamu ya sita ni sikivu hili nalo libebwe kwa upana mkubwa" alisema Anne Kilango. 



Mbunge huyo aliwaahidi  wananchi hao kuhakikisha analibeba swala hilo na kulipigania mpaka Bungeni kuhakikisha kituo hicho kinajengwa katika Kitongoji hicho ili kumalita tatizo la wananchi kuuwawa na Tembo kwani wanachohitaji wananchi kwa sasa ni ulinzi na usalama wao.



Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Maore, Issa Rashidi alisema kuwa, tatizo la mwananchi huyo kuuwawa na Tembo limemgusa kila mmoja na kuwaomba kuwa watulivu  hasa kipindi hiki ambacho Serikali inatafuta njia ya kumaliza tatizo hilo la Tembo kuvamia makazi ya watu.



Rashidi alitumia pia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya wanyama hao pamoja na kujijengea tabia ya kuwasindikiza watoto kwenda shule asubuhi na jioni kwenda kuwachukua ili kuepuka madhara pindi watakapokutana na Tembo. 



Aidha alitumia pia nafasi hiyo kuwaasa  wananchi wa Kitongoji hicho kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ili kumrahisishia yeye pamoja na mbunge kuwasemea matatizo yao kirahisi baada ya kujua idadi ya wananchi waliopo.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI