NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameendelea na ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kufanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Arusha Chini.
Mbunge aliandamana na Diwani wa Kata hiyo Waziri Mkakazi, Katibu wa Umoja wa wanawake (UWT), Shakila Singano, Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Kata ya Arusha Chini, mwakilishi wa Shirika la TANESCO Fredy Robert, na Mwakilishi wa shirika lisilo la kiserikali FTK ndugu Kuya.
Ziara ya Ndakidemi ilianza kwa kutembelea na kusalimiana na viongozi wa kiwanda cha Sukari cha TPC ambao ni wadau wakubwa wa maendeleo kwa Kata zinazozunguka kiwanda hicho.
Baadae Mbunge alikagua kivuko cha Samanga kilichopo katika jijiji cha Chemchem ambacho ni kero kubwa inayowakabili wakazi wa kijiji hicho pamoja na kuangalia bonde la kilimo la Chemchem.
Mbunge alijionea fursa kubwa ya kilimo cha umwagiliaji katika eneo hilo na kufurahishwa na shughuli za wananchi.
Akiwa katika kiwanda cha TPC, mwakilishi wa menejimenti ya kiwanda Yann Hardy alieleza kusikitishwa na kitendo cha baadhi ya wanasiasa kubariki na kuuzorotesha mradi wa kilimo katika kijiji cha Mtakuja.
Alisema kuwa mradi huo umepata fedha nyingi za ufadhili wa miundombinu ya umwagiliaji na umeme kutoka TPC kupitia shirika lake tanzu lisilo la kiserikali (FTK) ambapo ulikuwa ni msaada mkubwa kwa wakulima wa kijiji cha Mtakuja kuzalisha mazao kwa zaidi ya miaka 10.
Vilevile, wanakerwa na kitendo cha TRA kutoza kodi fedha za misaada zilizoelekezwa FTK kwa ajili ya maendeleo ya wanavijiji vilivyopakana na TPC na kudai kuwa fedha hizo ni za msaada wa kuiunga serikali mkono kutoa huduma kwa wananchi.
"Taasisi ya FTK imekuwa haifanyi biashara bali inawasaidia wananchi lakini inasikitisha pesa ya msaada kwa huduma za jamii kukatwa kodi" alisema Yann.
Katika ziara hiyo, Mbunge alikagua ghala la kuhifadhi mazao lililojengwa na serikali katika kijiji cha Chemchem na kutelekezwa bila kumalizika tokea mwaka wa 2017.
Viongozi wa Kata hiyo walimwomba Mbunge aiombe serikali ikamilishe mradi huo pia alitembelea ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Chemchem inayojengwa kwa msaada wa shirika tanzu lisilo la kiserikali la FTK lililoasisiwa na kiwanda cha sukari cha TPC.
Serikali kupitia halmashauri ya Moshi imepeleka shilingi milioni 50 kujenga jengo la mama na mtoto katika Zahanati hiyo na ujenzi uko katika hatua ya kukamilika.
Akisalimia wananchi, Katibu wa Umoja wa wanawake Wilaya (UWT), Shakila Singano aliwaambia Wanawake na Vijana kujiunga katika vikundi ili wapate fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri.
Aliwaambia kuwa ili kikundi kipatiwe mkopo kupitia mfuko wa maendeleo ya wanawake na vijana ni lazima kiwe kimesajiliwa na kumtaka Afisa Maendeleo wa Kata kutekeleza majukumu yake kwa kusaidia makundi hayo kupata mikopo.
Akimkaribisha Mbunge kuongea na wananchi, Diwani wa Kata ya Arusha Chini Waziri Mkakazi alieleza wananchi mafanikio waliyoyapata tokea waingie madarakani.
Alimweleza Mbunge kuwa changamoto yao kubwa ni kujengewa daraja la kuunganisha kijiji cha Chemchem na Mikocheni, na kuboresha miundombinu ya barabara.
Diwani alieleza kuwa wananchi katika Kata yake wamekuwa wakipata kipato kutokana na shughuli za kilimo, hivyo ni vyema wakajengewa skimu ya umwagiliaji ili kutumia vizuri maji ya mto Kikuletwa na yale ya mafuriko.
Alisema kuwa, kumekuwa na sintofahamu ya usalama kati wa Wakulima na Wafugaji kutokana na hali hiyo, mkuu wa wilaya ya Moshi Abas Kayanda ameridhia kituo cha polisi kujengwa katika kijiji cha Chemchem ili kukabiliana na uvunjivu wa amani unaotokea mara kwa mara.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliyofanyika katika viwanja vya zahanati ya Chemchem, ambapo Mbunge alisema kuwa kijiji cha Chemchem kinahitaji jicho la pekee ili kuwakwamua wananchi na matatizo yanayowakabili.
Katika mkutano huo, Mbunge alihamasisha wakazi wa Kata ya Arusha chini wajitokeze kila mmoja kushiriki katika sensa itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu kwani Serikali hutumia takwimu za sensa kupanga na kukadiria matumizi ya raslimali fedha kwenye kuwaletea maendeleo.
Prof. Ndakidemi alitumia mkutano huo kuelezea nia njema ya serikali ya awamu ya sita kuwaletea maendeleo na kudai kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameidhinisha shilingi milioni mia nne sabini na tano (475,000,000) ili kujenga barabara ya Samanga Chemchem kwa kiwango Cha Changarawe.
Alisema kuwa, barabara hiyo ilikuwa kilio cha muda mrefu na ikizingatiwa barabara hiyo ni muhimu sana, kwa kuwa ndiyo lango la kuingia kijijini ambapo Serikali ya awamu ya sita imeanza kutekeleza ahadi zake kwa vitendo.
Mbunge aliwaambia wananchi kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022, wakulima walinunua mbolea za kukuzia kama UREA kwa kati ya Sh 130,000 hadi 140,000 kutoka Sh 50,000 msimu wa 2020/21, huku mbolea nyingine za kupandia kama DAP ikinunuliwa kati ya Sh 120,000 hadi 130,000 kutoka Sh60,000.
Kutokana na kero hii ya kupanda bei ya mbolea, Serikali imetenga shilingi bilioni 150 ili kila mkulima aweze kupata mbolea yenye ruzuku kwa bei nafuu na kuwataka wananchi muda wa kujisajili ukifika wachangamkie fursa hiyo kwani bila kusajiliwa hawatapata mbolea ya ruzuku.
Akizungumza katika mkutano huo, Meneja wa Umwagiliaji wa Kanda ya kaskazini, Mhandisi Saidi alisema kuwa Wizara ya Kilimo imenuia kuwakomboa wakulima wa kijiji cha Chemchem kwa kuwajengea Skimu kubwa ya umwagiliaji itakayokuwa kichocheo cha kuzalisha mazao bila kutegemea mvua.
Amesema, serikali imeshatenga fedha za kufanya upembuzi yakinifu, kazi ambayo itaanza muda wowote hali iliyopokelewa kwa shangwe kubwa toka kwa wananchi ambapo kauli hiyo aliitoa akiwa anajibu hoja ya Diwani Mkakazi na wananchi waliohoji kuwa serikali ina mpango gani wa kutumia fursa ya kero ya mafuriko ya mto Kikuletwa kumwagilia mashamba yao.
Mwakilishi wa Shirika la Umeme TANESCO, Fredy Roberts aliwashauri wakazi wa Arusha Chini wajiongeze na kuunganishiwa umeme huku akidai kuwa bei ya umeme wa REA ni shillingi elfu ishirini na saba.
Alisema kuwa kijiji cha Chemchem kiliunganishwa katika mtandao wa TANESCO siku za karibuni lakini inashangaza wakazi wa eneo hili hawajaunganishiwa umeme.
Mwenyekiti wa kijiji cha Chambogo Kadoba alimweleza Mbunge kuwa Kata ya Arusha Chini inakabiliwa na changamoto kubwa ya Maji safi na Salama na kuomba ufanyike mchakato wa kutumia maji ya mto Kikuletwa kwa matumizi ya nyumbani ambapo Mbunge aliipokea changamoto hiyo na kuahidi kuifikisha kwenye mamlaka husika.
Akifunga kikao na kutoa maneno ya shukrani, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Arusha Chini alimshukuru Mbunge kwa kuwatembelea na kwa kuwapatia pesa kiasi shilingi laki 5 kutoka mfukoni mwake kusaidia ukarabati wa ofisi ya kijiji.
Mwisho
0 Comments