NA MATUKIODAIMAAPP, TANGA
BODI ya Mkonge Tanzania (TSB), imesema iko tayari kushirikiana na Falme ya Babina Noko Ba Mampuru iliyopo Jimbo la Limpopo nchini Afrika Kusini kuendeleza zao la mkonge.
Ushirikiano huo utakuwa katika mambo mbalimbali ikiwamo kutoa wataalamu wake na kubadilishana uzoefu baina ya nchi hizo mbili.
Kaimu Mkurugenzi wa TSB, Saddy Kambona amesema hayo mwishoni mwa wiki, wakati akizungumza na Mwana wa Mfalme wa Falme ya Babina Noko Ba Mampuru, Spumendo Mokgabudi aliyemtembelea ofisini kwake jijini Tanga.
Mwana wa Mfalme Mokgabudi, yuko nchini kwa ziara yake binafsi kwa ajili ya kufanya utafiti na kujifunza mambo mbalimbali kuhusu zao na kilimo cha mkonge akiwa na mpango wa kuanzisha kilimo hicho kwenye falme yake ambapo akiwa Tanga amekutana na Menejimenti ya Bodi ya Mkonge na uongozi wa Kampuni ya D.D. Ruhinda.
Katika mzungumzo yao, Mokgabudi amemuomba Kambona kumsaidia mambo matatu ikiwamo kuiomba Bodi ya Mkonge imsaidie upatikanaji wa mbegu za mkonge kwa ajili ya falme yake.
“Tumepata ugeni wa Mwana wa Mfalme kutoka Afrika Kusini, tumezungumza mengi lakini kikubwa ni kuhusu suala zima la zao la mkonge na miongoni mwa mambo aliyoomba mbali na upatikaji wa mbegu ni kubadilishana wataalamu ambao watakuja nchini na wa hapa kwetu kwenda kule ili kujifunza mambo mbalimbali kuhusu mkonge na mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo.
"Na jambo la tatu ni kusaidia utaalamu na miongozo mbalimbali itakayowezesha Falme ya Babina Noko Ba Mampuru kuanzisha bodi yake ya mkonge.
“Sisi kama Bodi ya Mkonge tumemuahidi ushirikiano lakini si tu na falme hiyo, bali Afrika Kusini kwa ujumla ambapo tutafikisha maombi hayo kwa wizara mama (Wizara ya Kilimo) ili taratibu nyingine ziweze kuendelea katika kusaidia falme hiyo kuendeleza zao la mkonge,” alisema Kambona.
Kwa upande wake Prince Mokgabudi, alisema atarudi wakati mwingine ili kujifunza kwa kuzunguka maeneo mengi zaidi kwani hii ni ziara yake binafsi nchini na katika mikakati ya kuanzisha kilimo cha mkonge nchini Afrika Kusini tayari wanazo hekta milioni tatu zilizotengwa kwa ajili hiyo.
“Nimekuja kujifunza kwa jicho la awali, nimejionea na nimejifunza mambo mbalimbali na nimevutiwa kuanzisha kilimo cha mkonge nchini kwetu kwani ardhi inaruhusu na hali ya hewa pia ni kama ya hapa.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya D.D Ruhinda Ltd. Deo Ruhinda alisema ushirikiano huo utaleta tija kwani kutakuwa na uhakika baina ya nchi hizo mbili.
“Ni uwekezaji mkubwa na mzuri ambao serikali ikiridhia hata sisi tutanufaika kwani chapa yetu itakuwa inatumika kama alama ya biashara. Ni mradi mkubwa ambao utakuwa na mambo mengi kama kupeleka mbegu na masoko lakini hatuwezi kuingia nao moja kwa moja bila serikali kutia mkono"alisema Ruhinda.
0 Comments