Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Mhandisi Robert Gabriel ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Bugando kwa usimamizi mzuri wa ukarabati wa Kliniki za Dharula na Ununuzi wa vifaa vya kutolea huduma mbalimbali chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Uviko 19 kwa Tshs Bilioni 3.9.
Amesema hayo leo Julai 5, 2022 wakati wa hafla fupi ya Uzinduzi wa majengo ya Huduma ya kwanza yaliyokarabatiwa na kufanyiwa upanuzi na kukabidhi kwa niaba ya Serikali vifaa kwenye vitengo vya wagonjwa Mahututi na dharula katika Hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando iliyopo jijini Mwanza.
Aidha, Mkuu wa mkoa amewataka watumishi wa Hospitali hiyo kutafsiri mapinduzi hayo makubwa kwa kutoa huduma za kibobezi kwa vitendo kwa kuongeza ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi na kuvitunza vifaa na mitambo ya kisasa kwa kuifanyia matengenezo kwa wakati ili iweze kudumu.
"Dkt Masaga umemtendea haki Mhe Rais Samia, kwakweli hongereni sana viongozi wa Bugando kwa kazi kubwa mliyofanya na sasa hospitali ya Bugando imekua ya Kimataifa na mmetafsiri kwa vitendo adhma ya Mhe Rais ya kutaka kuona wananchi wake wanapata huduma bora na za kisasa." Mkuu wa Mkoa amefafanua.
Mhe. Julius Peter, Katibu wa CCM Mkoa amewapongeza Bugando kwa usimamizi mzuri wa fedha hizo na kuhakikisha zinatumika kutimiza yaliyokusudiwa na ametoa rai kwa watumishi kuendelea kuwahudumia wananchi kwa kina katika kuokoa maisha yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Dkt. Fabian Masaga amemshukuru Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia Tshs Bilioni 32 zilizoelekezwa kanda ya ziwa katika kujenga Miundombinu na kuunua vifaa ambapo Tshs Bilioni 3.9 zimepokelewa Bugando kwa ajili ya ukarabati wa majengo na kununua vifaa.
"Maboresho haya ni makubwa sana, sasa tunakwenda kuhudumia wagonjwa wengi zaidi kwani kabla ya upanuzi huu tulikua na vitanda 27 lakini sasa tuna vitanda 51 kwa wagonjwa wa dharula upande wa watoto, kawaida na waliopasuliwa." Dkt Masaga.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya damu, Dkt. Thekla Mtobesya ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuwapatia mashine ya kisasa ya kutenganisha damu na viambata vyake huku akibainisha kuwa itawasaidia kukusanya damu pamoja na viambata vyake kama chembe nyekundu, sahani na nyeupe na kubadirisha chembe zenye ugonjwa na kubaki hazina ugonjwa.
Naye Bi Sofia Kassim, Muuguzi Idara ya Kuhudumia watoto Mahututi ambao hawajatimiza siku 30 tangu kuzaliwa amebainisha kuwa pamoja na vifaa vingine, Idara hiyo imepata vitanda 21 wakati awali walikua na vitanda kumi tu hivyo ameona mkono wa neema kutoka kwa Mhe. Rais Samia.
0 Comments