NA TITUS MWOMBEKI, MATUKIO DAIMA APP KAGERA.
Mkunga aliyesaidia kuzalisha mama wawili nje ya geti la zahanati ya Kashai iliyoko manispaa ya Bukoba mkoani Kagera baada ya wauguzi waliokuwa zamu katika zahanati hiyo kugoma kufungua geiti Bi. Leokadia Samweli amelishukuru shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutambua mchango wake na kuamua kumuunganishia umeme.
Ameyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari nyumbani kwake baada ya kuunganishiwa huduma ya umeme nyumbani kwake, huku akiwashukuru sana TANESCO, viongozi wa mkoa huo pamoja na uongozi wa kituo cha redio Kasibante kwa kumuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu tangu aliposaidia maisha ya mama hao.
“Namshukuru mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kufanikisha jambo hilo,naniwashukuru shirika la TANESCO kwa kuniangalia, kuniona na kuniinua na mimi nisifadhaike tena maana nilikuwa natumia kibatari ila pia namshukuru diwani pamoja na mbunge wa jimbo la Bukoba mjini aliyeagiza kutekeleza jambo hili leo nimeunganishiwa umeme”
Kwa upande wake afisa uhusiano na huduma kwa wateja shirika la TENESCO mkoa wa Kagera, Samweli Mandari amesema kuwa wamefanikiwa kumuunganishia umeme mkunga Leokadia Samaweli katika nyumba yake kutokana na maelekezo waliyopewa na Naibu Waziri wa Nishati na Umeme(MB) Steven Byabato.
“ Tarehe 25 mwezi huu tulipokea maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri wa Nishati na Umeme(MB) Steven Byabato, kwamba sisi kama TANESCO tunatakiwa kushiriki jambo hili kama kutoa mchango kwa jamii ambao ni utaratibu wa kawaida wa shirika kuweza kuchangia masuala ya kijamii, leo tunafurahi tumeweza kumuunganishia umeme bibi huyu ambaye alifanya tukio la kishujaa la kuwasaidia mama ambao walikuwa wamepata changamoto katika zahanati ya Kashai, na sisi tumemuunganishia umeme bure bila gharama zozote" aliasema Mandari.
Ameongeza kuwa TANESCO wamefanikisha huduma hiyo kwa kwa kutumia mfumo mpya wa NI-KONEKT unaowarahishia wateja kupata huduma kwa haraka zaidi hata akiwa nyumbani kwake kwa kutumia vifaa kama vile simu, kompyuta au kutembelea ‘website’ ya shirika hilo ambayo ni www.tanesco.co.tz.
Naye diwani wa kata ya Kashai iliyoko katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Ramadhan Kambuga amelishukuru shirika la TANESCO , viongozi wa mkoa wa Kagera, wadau mbalimbali pamoja na wananchi ambao wamejitokeza kutoa michango mbalimbali ikiwemo ya vifaa vya ujenzi wa nyumba ya bibi huyo ambayo ujenzi wake umefikia hatua nzuri.
Tukio hilo la kishujaa lililofanywa Bi. Leokadia Samweli la kuzalisha akina mama wawili nje ya geti ya zahati ya Kashai ilitokea Julai Mosi mwaka huu majira ya saa 10 alfajiri.
0 Comments