Na Gift Mongi, MatukioDaimaAPP MOSHI
Kutokana na mnyumbuliko wa kibiashara unavyozidi kwenda kwa kasi kampuni ya kutoa huduma za mazishi ya GodMark ya mjini hapa imeanzisha huduma ya kuchukua miili ya marehemu wanaofia nyumbani na kupeleka hosipitali kwa ajili ya kuihifadhi kusubiri taratibu nyingine za mazishi.
Huenda ubunifu huu ukawa ni wa kipekee kutolewa na kampuni hiyo ambapo utaweza kutoa msaada kwa watu wanaoishi ndani ya mkoa wa Kilimanjaro ambapo mtu akipatwa na umauti ataweza kufuatwa na na kusafirishwa hadi hosipitali iliyopo karibu kwa ajili ya kuusitiri mwili wa marehemu.
Lucas Gondwe ni mkurugenzi mwenza wa kampuni ya kutoa huduma za mazishi ya GodMark ambapo alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona wapo watu wanaopatwa na msiba na kukosa namna ya kwenda kumuhifadhi mpendwa wao wakati wakisubiri taratibu nyingine kutokana na maeneo wanayooshi.
Alisema huduma hiyo ambayo itapatikana ndani ya masaa 24 itawahusisha wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro ambapo mtu akipatwa umauti nyumbani ataweza kufuatwa na kusafirishwa tayari kwa kwenda kuhifadhiwa katika hosipitali ambapo wafiwa watahitaji mpendwa wao ahifadhiwe.
"Tumegundua wapo watu wanaopatwa na umauti wakiwa nyumbani lakini kunakuwepo na changamoto katika kwenda kuwahifadhi yaani mochwari zinakuwa mbali sasa sisi tutaenda kutoa huduma hiyo kwani wapo watu ambao hawawezi kulala na maiti ndani"alisema
Alisema kutokana na jiografia ya mkoa wa Kilimanjaro ilivyo si watu wote ambao wataweza kusafirisha maiti hususan nyakati za usiku lakini kampuni hiyo itawiwa kufanya hivyo kutokana na kuona umuhimu wa kusitiri miili marehemu.
"Tutapatikana kwa muda wote na lengo ni kutoa huduma na tumeona kuna hiyo haja kwani wengi wanapata taabu ila sisi tunaenda kuwarahisishia kwa kuusitiri mwili wa mpendwa wao kwa pale watakapotuhitaji tena kwa gharama nafuu"alisema
Kampuni ya GodMark mbali na kuja na huduma hii mapema mwaka jana ilikuja na huduma ya kulipia kidogogo kidogo jeneza ambapo itatoa ahueni pindi mtu anapofariki dunia ataweza kulipata bila kuleta usumbufu kwa njia yoyote ile.
Genes Mmasy mkazi wa Himo alisema huduma hiyo huenda ikawa ri rafiki zaidi kwenye jamii kwani mtu anapopatwa na umauti jamii hubadilika na kuwa vigumu au hata gharama kuongezwa ili kusafirisha marehemu kwa kuwa si jambo la kawaida.
"Mmiliki wa gari akifuatwa usiku akiambiwa ni maiti ya kupeleka mochwari anaongeza gharama ila hawa huenda wakawa na bei nzuri kwani wanatoa huduma na huenda ni jambo la kipekee kwetu sisi wanyonge"alisema
Mwisho.
0 Comments