Na Gabriel Kilamlya NJOMBE
Wakati zoezi la Anwani za Makazi likitakiwa kukamilika Mei 30 mwaka huu kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali, mkoani Njombe kumeripotiwa kuwapo kwa uhaba wa rasilimali chuma kinachohitajika kwa ajili ya nguzo za kusimika barabarani kama utambulisho wa barabara hizo na kulazimu kutumia nguzo za miti.
Hapa ndipo tunapoanza kuona umuhimu wa kuharakisha mradi mkubwa wa chuma cha liganga kilichopo wilayani Ludewa mkoani hapa kwani zoezi hilo limeonekana kukwamishwa na nguzo hizo za chuma licha ya kutumia mbinu mbadala kutekeleza zoezi hilo.
Kituo hiki kimefuatilia maendeleo ya zoezi hilo ambalo muda wake unafika ukomo mwezi huu wa Mei kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali ambapo katika mtaa wa Joshoni mjini Njombe Mwenyekiti wake Amon Swalle anasema wamelazimika kutumia nguzo za miti katika barabara zake kutokana na changamoto hiyo.
Wakazi wa mitaa mbalimbali Mjini Njombe akiwemo Eliza Mligo na Diana Paul wanakiri kuwa nguzo za chuma ni imara zaidi lakini uchumi kwao kimekuwa kikwazo.
Waziri Waziri Kindamba ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe ambaye amesema wamekutana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa zoezi hilo ikiwemo kuibiana namba za nyumba pamoja na nguzo za chuma huku wengine wakibandika namba eneo la kificho na Nyumba zao badala ya kubandika eneo la wazi kama ambavyo muongozo unataka.
0 Comments