Teddy Kilanga, Arusha
Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto amewataka watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na Wakaguzi wa Ndani mapema ili kudhibiti na kuondoa athari za vihatarishi katika taasisi wanazozisimamia.
Kauli hiyo imetolewa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto leo jijini Arusha kwenye ufunguzi wa mafunzo ya ukaguzi kwa kuzingatia vihatarishi (Risk Based Audit) kwa wakaguzi wa ndani 474 kutoka katika Taasisi, Wakala wa Serikali na Mashirika ya Umma 237 yaliyo chini ya Msajili wa Hazina.
Msajili alisema kwamba menejimenti ikisikiliza ushauri watawezesha kuwapo kwa udhibiti wa ndani mzuri utakaozuia ukiukwaji wa Sheria,Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyowekwa na hivyo kuiletea tija Serikali.
“Kunapokuwapo na udhibiti wa ndani imara Taasisi itafanya kazi zake kwa tija na kuwasilisha mapato yanayotarajiwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya Serikali, na pia kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Benedicto.
Pia amewataka Wakaguzi wa Ndani ambao amewaeleza kuwa ndio jicho kuyatilia maanani mafunzo hayo ili kwenda kuzisaidia taasisi wanazozikagua kwa kuwashauri juu ya kuimarisha udhibiti wa ndani.
“Ni imani yangu kwamba mafunzo haya yatawasaidia Wakaguzi wa Ndani na kuwajengea uwezo wa kufuatilia na kutekeleza kwa ufanisi taratibu mbalimbali za ukaguzi na kushauri kwa Maafisa Masuuli ipasavyo,” alisema.
Alisema ofisi yake ambayo ina jukumu la kusimamia Uwekezaji wa Serikali na kuishauri Serikali kuhusu masuala ya uendeshaji na uwekezaji katika Taasisi, Mashirika ya Umma, Wakala wa Serikali na Kampuni ambazo Serikali ni Mbia ilipanga mafunzo hayo kufuatia pendekezo la wakaguzi hao wakati wa mafunzo yaliyopita ya mfumo wa GARI ITS yaliyofanyika katika mwaka wa fedha wa 2020/21.
“Katika usimamizi wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala wa Serikali, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeona ni vema iendeshe mafunzo yanayohusiana na ukaguzi wa kuzingatia vihatarishi (Risk Based audit) kuwasaidia ninyi katika kuongeza uwezo wa utendaji kazi wenu wa kiukaguzi na kuleta tija katika ushauri na mapendekezo mnayotoa kwenye Taasisi zenu,” alisema Msajili.
Aidha, Msajili alitaka wakaguzi kuelimisha menejimenti juu ya kuzingatia vihatarishi na madhara yanayoweza kutokea iwapo vihatarishi havitazingatiwa na kudhibitiwa.
Msajili katika hotuba yake hiyo aliwapongeza wataalamu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina wakishirikiana na Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuandaa mafunzo haya ambayo ni sehemu ya kuimarisha mifumo ya ndani ya udhibiti na usimamizi wa fedha za Umma katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali.
Aidha, aliwashukuru wadau wa maendeleo wanaofadhili Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP) kwa kuwezesha kifedha kuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika.
Naye Mkaguzi Mkuu wa Ndani, CPA Magdalene Kirumba akimkaribisha Msajili wa Hazina kufungua mafunzo hayo alimshukuru kwa kutayarisha mafunzo hayo ambayo alisema ni muhimu kwa kuleta uelewa wa pamoja kuhusiana na dhana ya ukaguzi wa Ndani kwenye Mashirika ya Umma.
Alisema mafunzo hayo yataboresha ubora wa taarifa za ukaguzi na kupunguza hoja za ukaguzi kwenye sekta ya umma.
Alisema pamoja na kuwapa maarifa mapya, wakaguzi lengo jingine la mafunzo hayo ni kujenga uwezo kwa Wakaguzi wa Ndani kuhusu Miongozo ya Kimataifa (International Professional Practice Framework -IPPF) na namna ya kutumia miongozo hiyo katika kufanya kaguzi mbalimbali.
“Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya yatatatua changamoto za kutokuwa na matokeo yaliyotarajiwa katika kaguzi zinazofanyika (Audit approach) kwenye Taasisi, Wakala na Mashirika ya Umma,” alisema Kirumba.
Akielezea umuhimu ya mafunzo hayo Mkaguzi Mkuu wa ndani kutoka ofisi ya Msajili wa hazina,Magdalena Kirumba amesema mafunzo hayo yatasaidia kuleta uelewa wa pamoja wa ukaguzi katika sekta ya umma.
Nao baadhi ya wawashiriki mafunzo hayo wanaishukuru ofisi ya msajili wa hazina kwa kuweza kuandaa mafunzo hayo kwani yatakwenda kuongeza tija katika utendaji wao wa kazi
Inaelezwa kuwa wakaguzi wa ndani ndio jicho la taasisi hivyo jumla ya washiriki 474 kutoka katika taasisi,wakala wa serikali na mashirika ya umma wapatao 237 watajengewa uwezo wa kukagua kwa kuzingatia vihatarishi.
0 Comments