Na Andrew Chale Matukio Daima App, Dar
WIZARA ya Afya, kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo, inatarajiwa kuendesha zoezi la utoaji wa chanjo ya Polio kwa watoto walio chini ya miaka 5 kwa nchi nzima, zoezi linalotarajiwa kufanyika Mei 18-210 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Afisa Mradi wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Bi. Lotalis Gadau alibainisha kuwa, lengo la zoezi hilo ni kutoa chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 wapatao Milioni 10,567,805.
"Tayari chanjo zaidi ya Milioni 13, tumezipata na tutaendesha zeozi kwa siku Nne, Mei 18 hadi 21 mikoa yote kwa watoto wa chini ya miaka 5.
Zoezi litakuwa la awamu Tatu, kwa mwezi Mei, June, na Julai, lakini kutakuwa na wasimamizi wa Kitaifa katika mikoa yote kusaidia mikoa kuendesha kampeni." alisema Gadau.
Na kuongeza kuwa, zoezi hilo litaendeshwa nyumba kwa nyumba.
Aidha, Mpango wa Taifa wa Chanjo ulianzishwa mwaka 1975 huku ukiwa na Chanjo 12 zinazozuia Magonjwa wanazotoa hapa nchini.
Kuhusu Polio, ambao ni ugonjwa wa unaosababishwa na virusi vya Polio ambapo kwa kawaida unasababisha kupooza na baadae kifo, ambapo pia ugonjwa huu uathiri watu wa rika zote lakini watoto wadogo uathirika zaidi.
..ugonjwa huu hauna tiba, lakini unaweza tu kuzuiliwa tu kwa kupata chanjo ya matone ya Polio au ya sindano." alisema Gadau.
Ugonjwa huo wa Polio umekuwa na viashiria mbalimbali ikiwemo: Ulemavu wa ghafla, tepetepe kwa viungo kama mikono ama miguu, kulegea kwa kiungo kukosa nguvu, kushindwa kunyanyua miguu ama mikono.
Mtoto kushindwa kukaa, kushindwa kutembea/kuchechemea, kuvuta mguu na mengine mengi.
Aidha, kampeni hizo zinakuja kufuatia kuibuka kupatikana kwa mgonjwa, Lilongwe, Nchini Malawi mnamo Februari 17, mwaka huu hivyo, Wizara ya Afya Nchini ikaonelea kuchukua juhudi za haraka ilikulinda wananchi wake zaidi dhidi ya ugonjwa huo wa Polio hasa kwa watoto wadogo.
Mwisho.
0 Comments