Header Ads Widget

WAKAZI WA WILAYA NGORONGORO WAUNDA KAMATI YA KUMALIZA MIGOGORO YA ARDHI WILAYANI HUMO.



Na Teddy Kilanga MATUKIO DAIMA APP Arusha 

Katika jitihada za pamoja za kumaliza mgogoro wilayani Ngorongoro wakazi wa wilaya hiyo wameunda kamati ya takribani watu 60 ili kuwa kiungo kati ya jamii na serikali katika kutatua mgogoro  wa ardhi  katika tarafa ya Ngorongoro

Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa kimila,wanawake na wenyeviti kwa lengo kumaliza migogoro,Mwenyekiti wa viongozi wa kimila wilayani humo,Metui Oleshaudo alisema kazi kubwa ya kamati hiyo yenye mchanganyiko wa makundi mbalimbali itakuwa kiungo kati ya wananchi na serikali.

"Itakuwa kiungo kati ya wananchi na serikali katika kuelekea kutatua migogoro hii bila kuathiri pande zote mbili zinazovutana ambapo kamati hii imeanza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi katika vijiji vyote vinavyozunguka eneo lenye mgogoro wa kilometa za mraba 1500,"alisema Oleshaudo.


Aidha alisema mchakato wa kukusanya maoni kwa wananchi bado unaendelea hivyo wanategemea kukamilisha taarifa hiyo ndani ya wiki moja au mbili zijazo na kuwasilisha kwa viongozi wa juu wa serikali na kwa umma.

Mwenyekiti huyo alisema ikiwa mchakato huo wa kukusanya maoni ukiwa unaendelea wanaiomba serikali isitishe mikakati yoyote inayoendelea Ngorongoro na Loliondo kwa sasa ili kuweza kupata nafasi ya kukaa meza moja kwa ajili ya mazungumzo hapo baadaye.

Hata hivyo aliiomba serikali kuwa mchakato wa watu kuhama kwa hiari usitumike kama silaha ya kugawa jamii ya wanangorongoro.

Pia alisema wanampongeza Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Waziri Pindi Chana kuwa Waziri wa maliasili na utalii hivyo wanamuomba Waziri mteule kuzuia propaganda  zozote dhidi ya wakazi wa Ngorongoro hasa jamii ya kimasai.

Oleshaudo alisema kuwa wanamuomba Waziri Chana kusitisha michakato yote inayoendelea na kutoa nafasi ya kusikiliza jamii pamoja na kukataza vitisho na kamatakamata dhidi ya wanajamii,viongozi wa haki za kibinadamu wanaotetea jamii ya wanangorongoro.


Diwani wa  kata ya Nainokanoka na  viti maalum kutoka tarafa ya Sare, Edward Maura na Kijooli  Kakeya walisema wako tayari kushirikiana na serikali katika kuwabaini wakazi wa wilaya ya Ngorongoro halisi ili kulinda maslahi mapana ya serikali.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI