Header Ads Widget

VIFO VYA WANANDOA WAWILI MTAA WA BUNKANGO KAGERA VYACHUNGUZWA NA POLISI

Na MatukioDaima APP ,Kagera 

JESHI la polisi mkoani Kagera linaendelea na uchunguzi wa kubaini chanzo cha vifo vya wanandoa wawili wakazi wa mtaa  Bunkango kata Nshambya katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, ambao wamekutwa wamepoteza maisha katika chumba walimokuwa wamelala, usiku wa kuamkia jana.

Wanandoa hao ambao majina yao halisi hayakupatikana haraka huku mtaani wakijulikana  kama mama Osward na 

baba Osward, imedaiwa kuwa vifo vyao vimetokana na jiko la mkaa, lililowashwa na mwanamke kwa lengo la kupika chakula.

Mwenyekiti wa mtaa wa Bunkango, Anath Abas amesema kuwa alipata taarifa kuwa mtoto wa wanandoa hao anayesoma darasa la pili ameshindwa kwenda shule baada ya kugonga mlango wa chumba walimokuwa wamelala wazazi wake kwa muda mrefu bila mafanikio, ambaye aliamua kutoa taarifa kwa jirani.



Amesema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo alikwenda eneo la tukio na kwamba alipofika aligonga mlango haukufunguliwa, akaita kwa sauti hakuna aliyeitika, akaamua kuinama chini kuchungulia na kumuona mwanamke akiwa amelala chini sakafuni huku mume wake akiwa amelala kitandani.


"Niliamua kuwaita viongozi wenzangu pamoja na baadhi ya wananchi tukasukuma mlango kwa nguvu na kukuta tayari wanandoa hao wamepoteza maisha tukatoa taarifa polisi" amesema.


Naye diwani wa kata ya Nshambya ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Bukoba Godson Gibson amesema kuwa baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa mtendaji wa kata yake, alitoa taarifa polisi kwa hatua zaidi, na kutumia fursa hiyo kuwaasa wananchi wake kuacha tabia ya kupikia ndani.


"Taarifa zinasena kwamba mwanamke alirejea nyumbani usiku akawasha jiko la mkaa na kumenya ndizi, na kisha kuingiza jiko hilo kwenye chumba kisha wakafunga mlango na madirisha na kupumzika" Gibson.


Kaimu kamanda wa polisi mkoani Kagera, Maketi Msangi amekiri kuwepo kwa tukio hilo, na kwamba uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa vifo vya wanandoa hao vimetokana na jiko la mkaa lililowashwa na kuingizwa katika chumba walimokuwa wamelala.

Amesema kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha vifo vyao vimetokana na kuvuta hewa yenye sumu inayotokana na mkaa, lakini akadai kuwa wanasubiri uchunguzi wa kitabibu ili kujiridhisha kama kweli hicho ndo chanzo cha vifo hivyo, na baada ya hapo miili ya marehemu itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI