Adeladius Makwega ,Matukio Daima APP -DODOMA
Aprili 13, 2022 nilikuwa katika kjiji cha Butiama ambapo miaka 100 ya tangu mwalimu Julius Nyerere kuzaliwa ilifanyika huku mgeni rasmi akiwa Mzee wetu Mizengo Kayanza Peter Pinda. Mzee Pinda mjamaa nilikuwa sijamuona kwa miaka mingi kwa hiyo macho yangu yalibahatika kumuona kwa hisani ya kumbukumbu hii ya Mwalimu Nyerere.
Kwa hakika eneo hili la Butiama namna lilivyokaa ni vigumu mtu kuweza kupata usafiri wa moja kwa moja kuelekea Mwanza, Musoma au Dodoma. Msafiri anawajibu kutoka huko hadi Kiabakari hapo ndiyo barabara kubwa za kwenda katika miji hiyo mikubwa ilipo.
Kwa kuwa shughuli ziliisha saa saa 9 ya mchana kwa hiyo nilitafuta usafiri wa kunitoa hapo, ndugu mmoja aliniambia kuwa tuwaombe TBC wana basi lao kubwa, kweli tulipofika hapo maombi yetu yaligonga mwamba.
“Basi letu limejaa, mwingine akisema jamani huku nyuma kuna nafasi.”
Jamani kweli tunamuacha mwenyekiti wetu wa zamani wa RAAWU hapa Butiama?
Kweli mwenyekiti wa zamani wa RAAWU TBC niliachwa Butiama.
Tulizungumza na basi lingine ambalo lilikuwa la Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) walitukubalia huku nikijiuliza Mzee Nyerere kwanini barabara kubwa hakuzipitishia Butiama?
Nikiwa ndani ya basi hili ndogo nilibaini kuwa lilikuwa limewabeba wamamuziki kadhaa kutoka bendi mbalimbali za Tanzania wakiunda bendi hii moja kama Tanzania All Stars Band (zamani).
Nikiwa ndani ya basi hili kwa kuwa na mimi si maamuma wa muziki huu nilibaini alikuwapo Hassani Msumari, Ramadhani Muhoza, Edo Sanga, Abdalla Hemba, Andrew Sekiona, Saad Ally, Hosseah Mgohachi, Rashidi Sumuni, Mjusi Shemboza, Mwinyijuma Muumini na Dalila Msafiri ambaye alikuwa mwanamke pekee.
Safari hii ilikuwa nzuri sana siwezi kusema zaidi ya kama ningepanda basi la TBC maana ya huko siyajui lakini kwa hakika ndani ya basi hili uhondo niliufaidi mno. Japokuwa safari ilitumia saa zaidi ya 15 hadi Dodoma usiku mzima sikupata hata jembe ya usingizi.
Kwa kuwa mimi mara zote nimekuwa si mchoyo wa simulizi naomba leo kwa heshima ya wanamuziki hawa naomba nikusimulie simulizi moja kati ya simulizi 22 zilizosimuliwa basini.
Nikiwa nimekaa siti jirani na mlango wa kutokandani ya basihili mwnamauziki mmoja ambaye hakuwa Dalila Msafiri alisema kuwa jamani tunafanya kazi lakini mtu ukistaafu mmm huko vijiji kwetu kuna mambo.
Simulizi hiyo wakati inalisimuliwa tayari wale waliofunga Ramadhani walishafuturu na tulikuwa tunapita Mbuga ya Serengeti, huku giza likitamaraki.
“Katika kijiji kimoja kulikua na jamaa aliyekuwa akifanya kazi katika mbuga za wanyama, watu wengi walimtambua kuwa ndugu huyu alikuwa ni gemu wa mbuga hiyo huku akitajwa na nduguze kijijini kama mjuzi wa kupambana na wawindaji haramu.”
Ndugu huyu alifanya kazi katika mbuga hiyo kwa miaka kadhaa na ulipofika wakati wa kustaafu alilipwa kilicho chake na kuamua kurudi kijijini kwao. Msimuliaji huyu aliendelea kusimulia huku basi hili likipita kwa kasi mbuga hii ya Serengeti.
“Kutokana na mazoea ya kufanya kazi kila siku na kuamka kwenda kazini, ndugu huyu alitamani kuwa na kazi ambayo itamsaidia ili awe bize kama yupo kazini.”
Kwa hiyo msimuliaji huyu alisema kuwa jamaa alitamani kuwa mwenyekiti wa kijiji ili awe bize na utatuzi wa migogoro ya kijijini. Kwa hiyo alimfuta mwenyekiti wa kijiji aliye madarakani ili amuachie nafasi.
Kweli mwenyekiti aliye madarakani alimwambia kuwa ombi lake amelisikia lakini hapo kijijini hakuna uenyekiti wa ubwete (bure).
Jamaa alimwamabia, sasa mwenyekiti aliye madarakani ampe hekima zake katika jambo jambo hilo.
Mwenyekiti aliye madarakani kwa kuwa alikuwa anahitaji wasomi washike nafasi ya uenyekiti kijijini hapo hakuwa na hiana alimwambia arudi nyumbani kwake na aje baada ya majuma mawili hekima itakuwa imepatikana.
Jamaa alirudi nyumbani kwake huku ulevi wa kuamka asubuhi na kwenda kazini ukiwa umemuingia damuni mithili ya mvinyo isiyoonekana kutoka katika utumishi wa umma aliyoufanya kwa miaka 27. Kwa majuma mawili yalikuwa sawa na miezi sita kijijini hapo.
Huku wanakijiji wenzake wakiendelea na maisha yao kama kawaida na jambo hilo likimstajabisha mno ndugu huyu. Mwishoni mwa juma la pili huku juma la tatu likikaribia kuanza mgambo wa kijiji hicho alitumwa na mwenyekiti kumfuata mstaafu huyo.
Mstaafu huyu alifika kwa mwenyekiti kuitikia wito, mwenyekiti akamjulisha ndugu huyu mstaafu kuwa kuna taarifa ya simba kuonekana katika mipaka ya kijiji chao. Kwa kuwa alikuwa akifanya kazi mbuga za wanyama basi anawajibu wakumsaka na akifanikiwa kumuua atakabidhiwa uenyekiti wa kijiji.
Baada ya makubaliano hayo mwenyekiti aliitisha mkutano wa kijiji na kuwaeleza tukio hilo la simba huku wanakijiji kukaa kwa tahadhari huku ndugu zao wakiingia msituni kumsaka simba huyo.
“Huyu ndugu yetu amestaafu ugemu serikalini, kwa hiyo ni hodari mno wa kupambana na wanyama wakali katika mbuga sebuse huyu simba mmoja wa ualani? Katika kazi hii anaambatana na wanamgambo watano wa kijiji kumsaidia.”
Mwenyekiti aliwahakikishia wanakijiji wake.
Kweli safari ilianza na kuelekea kumsaka simba huyo kabla ya kuleta madhara kijijini. Kwa hiyo kikosi cha watu sita kilianza safari hadi msituni wakimsaka simba huyo.
Walizunguka zunguka wapi siku ya kwanza, ya pili hivyo hivyo hadi siku ya sita jioni waliamua kupanda juu ya miti kupumzika, kandoni kukiwa na mto unaopitisha maji ambapo wanyama kadhaa hunywa.
Kabla ya kupanda juu ya miti hiyo walikula posho zao za mabumunda na asali wakanywa maji na kupanda juu ya miti mikubwa sita.
Wakiwa wamelala juu kila mmoja na gobore lake kwapani walipatwa na uzingizo mzito lakini kijana mmoja wapo alikuwa macho. Simba alifika pale walipolala na kujilaza chini ya mti wa yule ndugu ambaye aliyekuwa akifanya kazi mbuga za wanyama.
Kijana aliyekuwa macho alidhani anaota, aliyafungua macho yake vizuri akamuona simba dume amejilaza kwenye kisiki cha mti mmoja, akawasitua wenzake kwa lugha ya ishara.
“Yupo(simba) chini ya mti.”
Yule ndugu ambaye alikuwa mstaafu kutokana na woga wa kumuona simba alichanganyikiwa huku kila kitu kikimtoka hapo hapo juu na kumuangukia simba yule naye simba kutimka mbio mgongoni akiwa mstaafu huyu.
Mstaafu alikamata masikio na nywele za simba dume huku akitambua kuwa akimuachia basi ataliwa hapo hapo, naye simba akifuata maelekezo ya jamaa mstaafu juu ya mgongo wa simba.
Wenzake walishuka juu ya mti na magobore yao wakachukua na gobore la mstaafu huku wakimkimbiza simba ambaye walidhani kuwa mwenzao analiwa sasa.
Kwa mbali huku wakikimbia walibaini kuwa walimuona simba akiwa amembeba mwanzao huku wakitaka kutupa risasi wakiogopa kuwa inaweza kuleta madhara kwa mwenzao. Wakidhani kuwa mwenzao alisomea namna ya kumpanda simba huku akiwa hai.
Simba na abiria wake mstaafu huyo walikuwa mithili wa dereva wa pikipiki aliyekuwa akikata mbuga porini. Simba huyo aliongozwa na ndugu huyu hadi kwa mwenyekiti.
“Mwenyekiti, mwenyekiti, mwenyekiti nimemleta mzima mzima!”
Mweyekiti akasema ebo,unasemaje ? Mwenyekiti nimemleta mzima mzima!, Acha mambo yako bwana mimi nilisema mlete akiwa amekufa.
Kwanza uenyekiti umeshaupata, rudi nae huko huko porini.
Kweli jamaa alimuelekeza simba huyo vizuri katika mwembe ambao mikutano ya kijiji inafanyika simba huyu alijigonga katika kisiki hicho na kufa hapo hapo.
Wenzake walioambata naye walipofika hapo wakashangaza walichokiona kikitokea, mstaafu nayeye haamini kilichotokea.
“Jamani mie mwenzenu katika mbuga za wanyama sikuwa gemu bali nilikuwa mpishi tu.”
Mstaafu alisema. Jamaa wenzake wakisema kama mpishi tu wa mbuga za wanyama mambo yako hivyo, vipi kwa gemu wenyewe?
Mbiu ya mgambo ilipigwa na wanakjiji waliwapongeza kwa kufanikisha kumuua simba na ndugu huyu kukabidhiwa uenyekiti wa kijiji.
Ama kweli hakuna uenyekiti wa ubwete.
Mwanakwetu safari ya kutoka Butiama kwenda Dodoma ilifika mwisho na mie kushuka Njia Panda ya Chamiwno Ikulu (Buigiri) na wanamuziki hawa kuendelea na safari yao kwenda Dar es Salaam.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments