Na Adeladius Makwega-DODOMA
Utaratibu wa elimu wakati huo ulikuwa unatoa nafasi mara baada ya bodi za shule za sekondari kumfukuza mwanafunzi kukata rufaa kwa bodi ya rufaa ya mkoa, na kama maamuzi ya bodi ya rufaa yasikubaliwa na upande wowote ule kati ya pande mbili ,shauri hilo linapelekwa kwa waziri wa elimu kama rufaa na kama kwa waziri elimu kuna upande hautoridhika shauri hilo linapelekwa mahakamani.
Kumbuka baba wa mwanakwetu alipotoka kwa dada yake wa Sokoni Kariakoo walikubaliana kuitana kikao cha wanandugu kulijadili jambo hilo kwa kina, kumbuka yule shangazi wa mwanakwetu anayefahamika kama Salome alikuwa akifanya kazi Sokoni Kariakoo, Kariakoo ndiyo ilikuwa sehemu ya wajanja wengi wa Dar es Salaam.
Huyu Salome ambaye ni shangazi wa mwanakwetu zamani alisoma Kisutu Sekondari akiwa anatokea Mbagala miaka ya sabini na alipokuwa msichana kwa maisha ya vijana wakristo yalikuwa ni kuhesimu mno dini kwa hiyo alikuwa akiimba kwaya ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Antony wa Padua Mbagala Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakati huo jimbo hilo lilikuwa linaongozwa na Kadinali Lauriane Rugambwa kadinali mmoja mrefu sana, mkali na mwembamba mweusi.
Wakati wanaimba kwaya hiyo sauti ya kwanza, sauti ya pili, ya tatu na ya nne walikuwa wakimba na vijana wenzao kadhaa wenyeji na wageni wa Dar es Salaam. Mwalimu wao wa kwaya hiyo alikuwa kijana kutoka Upimbweni Peter Pinda(Mizengo Pinda). Kwa maelezo ya wanakwaya kadhaa walio hai hadi leo wanasema kuwa wao walimfahamu Peter kama hakimu.
“Mwalimu wetu wa kwaya yeye ni hakimu na kabila lake ni Mpimbwe.”
Kwenye kikao cha wanandugu hao Salome aliwaambia nduguze kuwa atamuomba Peter ili asaidie katika shauri hilo kwa kutuandikia rufaa, lakini kwa kuwa alikuwa na namba yake ya simu ya nyumbani atakwenda kazini Sokoni Kariakoona kudoea simu ya ofisini kwak kumpigia simu na kumueleza, alafu atakachomwabia atawaeleza nduguze.(Msomaji wangu kumbuka hiyo 1993 simu za mkononi hazipo).
Alipozungumza naye ndugu Peter (mwalimu wake wa kwaya wa zamani wa Kwaya ya Parokia ya Mbagala) alisema kuwa mwambie huyu mwanafunzi aje kwangu Msasani nyumba namba 55 na barua husika, na ripoti zake zote za taaluma tangu kidato cha kwanza hadi kidato cha tatu.
Kweli mwanakwetu alipoelezwa alipanda basi hadi Stesheni, hapo alikutana na basi la UDA kila baada ya saa moja linakuja la kwenda Msasani, na daladala zilikuwa haziendi Msasani.
Nilipanda UDA hiyo hadi Morogoro Stoo na kushuka na Barabara ya Kaunda hadi Msasani nyumba namba 55. Nyumba hiyo ya serikali ilikuwa ni kawaida tu hakukuwa na geti wala nini bali palikuwa na uzio wa miti ya kawaida ya kupandwa, hakukuwa na ulinzi wowote ule.
Nadhani ndugu Peter alikuwa mtumishi wa serikali mkubwa kwa kuyatazama tu yale maeneo aliyokuwa akiishi na majirani zake, binafsi sikuwezi kutambua cheo chake. Kwa muda niliyokuwa naenda nilibaini kuwa alikuwa mfugaji wa ng’ombe wa kisasa, kuku wa kisasa na kienyeji na alikuwa akilima bustani ya mboga mboga na majirani zake wengi walinunua maziwa, kuku na mbogamboga kutoka kwake.
Nyumbani hapo japokuwa mwanakwetu alifika kwa muda mfupi sana alibaini kuwa ndugu Peter Pinda kwa upande wa kulia alipakana na Jaji Mkude katika nyumba hii ya jaji huyu ndipo alipokuwa akiishi mwanamuzi Mr Paul, nyumba inayofuata alikuwa akiishi Jaji Kiongozi wa wakati huo Marehemu Augustino Ramadhani kwa jaji huyu Mzanzibari mbele yake kulikuwa na kibanda kidogo kama kioski kilichouzwa soda.
Nyumba hii ndugu Peter pia ilitazamana na ghorofa moja dogo ambalo alikuwa akiishi Nsa Kaisi ambaye nadhani alikuwa mkuu wa mkoa, Nsa Kaisi yeye alikuwa kidogo mambo mazuri maana alikuwa na Jenereta kubwa hata umeme ukikatika linawashwa.
Mbele ya Peter Pinda palikuwa na nyumba nadhani ni nambari 54 hapa alikuwa anaishi Brigedia Kotta wakati huo nadhani alikuwa bado Jeshini na alikuwa na ulinzi wa jeshi. Kwa wale ambao hawamfahamu vizuri Brigedia Kotta alikuwa Mkuu TALK AIDS na huyu ndiye Baba wa Faraja Kotta yule mrembo wa mjini, mrembo Dar es Salaam, mrembo aliyekulia jirani na bahari, ambaye alikuwa akioga maji ya bahari na mambo ya maji ya bahari si unajua msomaji wangu, maji yake yana chumvi chumvi hata mabaya hayakukuti kama unayaoga. Hiyo ndiyo sifa ya bahari na huyo ndiye Faraja Kotta(Mrembo).
Hapa kwa Brigedia Kotta palikuwa shule ya Chekechea iliyofahamika kama Faraja Day Care Center, shule hii ilikuwa inasimamiwa nadhani na mke wa Brigedia Kotta ambaye ni mama wa Faraja Kotta (Mrembo). Mama huyu aliwahi kufundisha Tambaza zamani kwa hiyo alikuwa akiutumia ualimu wake nyumbani. Huku shule yake ikiwa na runinga na akifundisha matamshi ya kiingereza kwa sauti za video kwa watoto.
Sifahamu kama Faraja Day Care Center inaendelea au la, nachokumbuka tu ilibeba jina la mtoto wa mwisho wa Brigedia Kotta ambaye ndiye mrembo Faraja Kotta. Sifahamu alipo mrembo huyu kwa sasa, kwa maana haya ninayoyasimulia ni ya kitambo, usione gere msomaji wangu na hata wakati huo Faraja Kotta alionekana mrembo. Hata sie wanafunzi wa Tambaza tulimtambua binti huyu kuwa ni mrembo. Maana mwenyezi Mungu ametupa macho ya kuona na kweli tuliutambua urembo wa Faraja Kotta lakini pia Mungu hakatuka na moyo … Sifahamu alipo Faraja Kotta kwa sasa ! lakini Kweli Faraja Kotta ni Mrembo.
Nitaulizia kwa binamu yangu mmoja aniambie alipo Faraja Kotta na je shule Faraja Day Care Centre inaendelea ili nimpeleka mwanangu akasome. Maana habari za Chekechea hii ni ndefu sana.
Mbele ya nyumba ya Brigedia Kotta palikuwa na Ecole de France hii shule ya msingi ya Wafaransa alafu unavuka barabara nadhani barabara ya Kaunda unakutana na Oyester bay Hotel nadhani ilikuwa ni mali ya umma wakati huo.
Nilipofika kwa ndugu Peter nikaribishwa na makochi ya rangi nyekundu, pakiwa na runinga kubwa. Nilikaa katika makochi haya huku pengine nikichafua zuria nadhifu la rangi nyekundu na vumbi na matope kutoka Mbagala.
“Mbona mnafanya vurugu shuleni? Tambueni kuwa miaka ya shule ni michache sana katika maisha lakini ina maana kubwa katika maisha ya binadamu.”
Alisema ndugu Peter Pinda.
Mwanakwetu alisimulia kilichotokea huku ndugu Peter akinukuu kwa kutumia note book yake, mazungumzo hayo. Maungumzo hayo hayakutumia zaidi ya dakika 10. Ndugu huyu aliomba kutajiwa majina ya marafiki watatu wa mwanakwetu akiwa shuleni Tambaza na jina la mwalimu wa darasa wa zamani kwa wale walimu wa mwanzo kabla hawajahamishwa.
“Ibrahimu Liguo (sasa ni mtumishi wa Wizara ya Mipango na Fedha), Hamisi Ramadhani (Rashidi Kazyoba) huyu alikuwa anakaa Mbagala ni yule ambaye nilikwenda naye kusoma tution tuliyotakiwa kusali msikitini na mtu wa tatu alikuwa ni Atanas Luis (Mzee Ole).”
Aliyaandika majina yao na kuniambia wafuate, wape ujumbe huo, na uje nao kesho saa 11 jioni.
Je wadau hao watakubali kwenda kwa ndugu Peter?
Subiri matini ijayo.
makwadeladius @gmail.com
0717649257
0 Comments