Teddy Kilanga, MANYARA
Shirika la World vision Tanzania kupitia mradi wa Ruvuru met (AP)umetoa chakula chenye thamani ya sh.milioni 148.2 katika tarafa ya Ruvuru met wilayani Simanjiro mkoani Arusha kwa lengo la kuongeza ufaulu kwa wanafunzi shuleni.
Aidha Wazazi na walezi wa wilayani humo wametakiwa kuzingatia lishe bora kwa watoto wao ili kuboresha ustawi wa mtoto pamoja na kuongeza ufaulu shuleni kupitia upatikanaji wa chakula katika shule mbalimbali zilizipo wilayani humo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi chakula kilichotolewa na shirika World vision Tanzania kupitia mradi Ruvuremit (AP)katika shule tisa zilizopo katika tarafa ya Ruvuremit wilayani humo,Mkuu wa wilaya ya Simanjiro,Dk.Suleiman Serera alisema moja ya mikakati ya kuongeza kiwango elimu ni upatikanaji wa chakula shuleni.
Aidha Dk.Serera alisema mwanafunzi anapopata chakula cha kutosha shuleni hupata nguvu za kusoma kwa bidii lakini anapokabiliwa na njaa ni rahisi kushawishika kutoroka shule hali ambayo inarudisha nyuma maendeleo yake ya elimu.
"Wenzetu Word vision Tanzania wametumia fedha nyingi kuleta chakula hiki katika shule zetu zilizopo Tarafa ya Ruvure miti ambapo ni ndani ya miezi mitatu mfululizo hivyo nawasisitiza wazazi na walezi msibweteke ni vyema mkajipanga kuhakikisha upatikanaji wa chakula shuleni unaendelea siku zote,"alisema Dkt.Serera.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Simanjiro,Christina Marwa alisema kupitia hali ya mabadiliko ya hali ya hewa iliyoikumba wilaya hiyo ni suala la kujifunza kwa wazazi na walezi kutoa maeneo ya mashamba ya shule ili kusaidia hupatikanaji wa chakula kwa wanafunzi pale inapotokea changamoto kama hiyo.
"Mnapotoa maeneo ya mashamba kwa ajili ya shule mnatakiwa kuwa na mkakati wa kudumu katika kuhakikisha chakula katika shule zetu kinapatikana kwani wamiliki wa shule ni wananchi hivyo inatupasa sisi sote kushirikiana kuhakikisha watoto wetu wanasoma pasipokuwa na kikwazo cha njaa,"alisema Marwa.
Alisisitiza kuwa endapo maeneo ya mashamba ya shule yakapatikana watakao kuwa wanalima ni wazazi kwa kutenga siku moja ndani ya wiki kwa ajili ya kulima lengo ni kuhakikisha watoto shuleni wanakuwa na ustawi bora pasipokuwa na kikwazo cha njaa.
Naye Mwezeshaji wa mradi Ruvure miti(AP)wa shirika la word vision Tanzania ,Aizack Mwaijande alisema chakula hicho watatoa ndani ya miezi mitatu ambapo kitagharimu zaidi ya sh.milioni 148.2 kwa watoto 3696 ikiwa mahindi tani 50.7 ,maharage 27.6,mafuta ya kula lita 2220.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ngage ni mmoja wa wanufaika wa shule yake kupata msaada huo wa chakula,Evans Mtalo ameshukuru shirika hilo kwani wamewasaidia wao katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji hapo shuleni unaozingatia upatikanaji wa chakula kwani kwa kipindi cha mchana watoto hawawezi kusoma na wanakuwa wanalegea kutokana na kukabiliwa na njaa.
"Watoto wanashindwa kupokea vipindi vya mchana kwani asubuhi huwa na nguvu lakini kadri muda unavyoenda ndipo kasi ya kujifunza inapungua hivyo tunawaomba wazazi wasibweteke bali tujipange suala la upatikanaji chakula shuleni liwe endelevu,"alisema Mwalimu mkuu huyo.
Baadhi ya wazazi walisema hapo awali walikuwa wanatoa chakula shuleni kwa ajili ya watoto wao lakini kwa bahati mbaya uchumi wao uliyumba kutokana na janga la ukame lililosababisha mifugo kufa na kupelekea kushindwa kuendelea na zoezi hilo.
Wakisimulia adha waliyokuwa wanapata baadhi ya wanafunzi shuleni ni kuchoka na kusinzia hali inayowapelekea kutoroka vipindi vya shule kutokana na njaa wanayohisi katika nyakati za mchana.
0 Comments