-Ni kupitia ndege zake, abiria Milioni 90.2 kutazama
Na. Mwandishi Wetu, Dubai.
SERIKALI ya Tanzania kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amefanya mazungumzo na Uongozi wa juu wa Shirika la ndege la Umoja wa Falme za Kiarabu la Emirates kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania ambapo vivutio hivyo vya utalii vitaweza kuonwa na abiria wapatao milioni 90.2 ambao husafiri kila mwaka kwa kutumia ndege hizo.
Aidha, Dkt.Ndumbaro amesema, Tangazo hilo litakuwa likitazamwa na mamilioni ya abiria hao kila wakati ndege za Shirika hilo zitakapokuwa zikiruka (take off).
Dkt.Ndumbaro amebainisha hayo leo katika Mji wa Dubai alipokutana viongozi wa Shirika hilo ambalo mbali ya kusafirisha abiria milioni 90.2 duniani kote pia husafirisha abiria wapatao milioni 20 ambao huunganisha ndege nyingine.
Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana kutaandaliwa makala tano (Documentaries ) za kuelezea vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo Zanzibar, Serengeti, Ngorongoro pamoja na Mlima Kilimanjaro .
'' Shirila la ndege la Emirates ni Shirika kubwa sana Duniani lengo letu kama nchi ni kuhakikisha abiria wapatao milioni 90.2 wanaviangalia vivutio vyetu kisha wanavipenda halafu wanatembelea Tanzania'' amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Katika mazungumzo hayo amesema Uongozi wa ndege hizo umeonesha utayari wa kushirikiana katika kuitangaza Tanzania kiutalii na ifika mwanzoni mwa mwezi wa tano mwaka huu wataingia makubaliano (MOU) baina ya Tanzania na Shirika hilo
Akifafanua mazungumzo hayo Dkt.Ndumbaro amesema kati ya abiria watakaoangalia vivutio wengi wao watavutiwa na hatimaye sehemu ya watu hao waweze kuja kutembelea Tanzania.
"Shabaha yetu kubwa kama nchi ni kuhakikisha tunafikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025, Tunaamini tutalifikia lengo hilo" amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Ameongeza kuwa Tanzania inategemea utalii wake wa Wanyamapori kwa asilimia 100 hivyo kupitia mkakati wa kutumia wa kutangaza vivutio vingine vya utalii kama vile utalii wa fukwe, utalii wa utamaduni pamoja na utalii wa ikolojia utaweza kujulikana dunia kote na kuwa chachu ya watalii wengi kuanza kumiminika nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Masoko wa Afrika wa Shirika la ndege la Umoja wa Falme za Kiarabu la Emirates, Badr Abbas amesema Shirika la Emirate lipo tayari kufanya kazi na Tanzania katika kuhakikisha vivutio vya utalii vya Tanzania vinajulikna pande zote za Dunia.
''Tutakapofikia makubaliano tutahakikisha pia matangazo ya vivutio vya Utalii wa Tanzania vinawekwa kwenye Tovuti pamoja na mitandao ya kijamii ikiwemo facebook, instagram pamoja na twitter ya Shirika hili ambayo imekuwa ikifuatiliwa na watu wengi Duniani,
Kwa upande wake, Balozi Mdogo wa Dubai, Mhe. Idd Bakari amesema mazungumzo yamekuwa na tija na hivyo kupitia Shirika hilo idadi ya watalii itaongezeka kupitia matangazo yatakayokuwa yakiruka wakati ndege za Shirika hilo zitapokuwa zikiruka
''Mazungumzo haya baina yetu na Shirika la Emirates yataipaisha Tanzania vivutio vya utalii vitaweza kujulikana Duniani kote kuwa vipo Tanzania na hivyo watalii wengi watweza kuitembelea Tanzania.
Katika mazungumzo hayo Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro pamoja na Balozi Mdogo wa Tanzania, Mhe.Idd Bakari
0 Comments