Header Ads Widget

RAIS SAMIA ANATARAJIWA KUZINDUA MRADI WA MAJI WA TSH BILIONI 18

 


RAIS Samia Suluhu Hassan Machi 22 anatarajiwa kuzindua mradi wa maji wa wenye thamani ya shilingi bilioni 18.


Mradi huo wa Mlandizi-Mboga- Chalinze utazinduliwa kwenye eneo la Msoga utakaohudumia baadhi ya wananchi wa wilaya za Kibaha na Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo.



Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge  akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha alisema mradi huo ni moja ya miradi mikubwa mkoani humo.


Alisema kuwa Rais atazindua mradi huo ikiwa ni sehemu ya kilele cha wiki ya maj na ni mradi huo wa bomba kuu kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) unatarajiwa kusafirisha kiasi cha lita za ujazo milioni 9.3 kwa siku.


Aidha alisema kuwa mradi utazalisha maji ambayo yatawezesha kuwahudumia wakazi wapatao 120,912 kwa siku.


"Uzinduzi wa mradi huo ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji ambapo katika mradi huo kuna vituo vidogo kwenye maeneo ya Chamakweza na Mboga ambapo zimefungwa mashine,"alisema Kunenge.


Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo wa bomba la kusafirisha maji lenye kipenyo cha inchi 16 umbali wa kilometa 59 kutoka Mlandizi (mitambo ya Ruvu Juu) hadi Kijji cha Mboga Chalinze kumesaidia kuondokana na adha ya ukosekanaji maji katika maeneo ya Wilaya za Kibaha Vijijini na Wilaya ya Bagamoyo.


"Baada ya kuzindua mradi huo atazungumza na wananchi Chalinze kwenye uwanja ulioko nyuma ya kituo cha Polisi Chalinze ambapo watu 5,000 watahudhuria,"alisema Kunenge.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI