Naibu Waziri wa Kilimo Mh Anthony Mavunde amewataka wakala wa mbegu za kilimo (ASA) kuhakikisha wanaweka uzio katika mashamba yao yote ya uzalishaji mbegu ili kutunza maeneo hayo kutovamiwa na wanyama na uvamizi wa shughuli za kibinadamu.
Hayo yamesemwa jana wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mavunde kutembelea maghala ya uhifadhi mbegu na mashamba ya uzalishaji mbegu katika Wilaya ya Morogoro Mjini na Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
“Tafiti zinaonyesha ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu Tanzania itaongezeka maradufu nyuma ya Nigeria na Ethiopia,hivyo basi Mahitaji ya chakula yataongezeka zaidi na njia ya kujihakikishia usalama wa chakula ni pamoja na kuwa na maeneo yaliyotunzwa kwa ajili ya Kilimo cha mazao ya chakula pamoja na uzalishaji wa mbegu bora.
ASA hakikisheni mnayalinda maeneo haya ya mashamba 14 ya uzalishaji mbegu kwa kuweka uzio ili kuwa na benki ya ardhi ya kutosha ya kuzalisha mbegu lakini pia kuzuia muingiliano na wanyama na shuguli za binadamu unaoweza kuathiri ubora wa mbegu mnazozalisha.
Hapa Msimba yapo maelekezo ya Mh Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwagawia wananchi ekari 1000 kwa ajili ya matumizi yao mbalimbali,nakushukuru Mh DC kwa usimamizi mzuri wa hili jambo na linakwenda kukamilika bila athari yoyote.
Nakupongeza Mtendaji Mkuu Dr.Sophia Kashenge pamoja na timu yako kwa kazi kubwa unayofanya ya kufufua na kufungua mashamba haya ambayo yameongeza maradufu uzalishaji wa mbegu bora kwa wakulima wetu,endeleeni kushirikiana na sekta binafsi ili tuzalishe mbegu nyingi zenye ubora kufikia tani 300,000 mwaka 2025 kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM inavyoelekeza”Alisema Mavunde
Naye Mtendaji Mkuu wa ASA Dr. Sophia Kashenge amesema kwamba kwasasa wamejipanga kuhakikisha uzalishaji wa mbegu mbalimbali bora unaongezeka nchini na kwasasa wanaelekea katika mpango wa kuweka miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji katika mashamba ya mbegu badala ya kutegemea maji ya mvua katika baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa ni kikwazo cha ufanisi hasa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
0 Comments