Na Gift Mongi, Moshi.
Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira mjini Moshi(MUWSA)imefanya ugatuaji wa majukumu yake na kuyashusha katika ngazi ya chini kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma nyinginezo.
Ugatuaji wa madaraka hayo baadhi yake yamekasimishwa kwa maafisa watendaji wa kata zinazohudumiwa na mamlaka hiyo ambazo 12 zinapatokana katika halmashauri ya Moshi wakati nyingine 21 zipo Manspaa ya Moshi
Afisa uhusiano wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Moshi(MUWSA)Flora Nguma alisema mamlaka hiyo kupitia mkataba wa huduma kwa mteja unaeleza wazi kabisa kuwa mteja atakuwa na haki zipi pindi akiwa mteja na kama zikikiukwa afanyeje
"Huu mkataba wa huduma kwa mteja ni kama kiunganishi kati yetu sisi kama mamlaka lakini na watu tunaowahudumia hii pia ni njia mojawapo yabiwajibikaji kwa jamii" alisema
Alisema kuwa mkataba huo umekuwa ukimalizika kila baada ya miaka mitatu na pindi unapotengenezwa mwingine mbali na kuwa shirikishi lakini pia huboreshwa kulingana na mahitaji ambayo jamii inataka.
Kwa mujibu wa afisa uhusiano huyo ni kuwa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Moshi ni taasisi ya kiserikali yenye jukumu la kusambaza majisafi na uondoaji majitaka katika manspaa ya Moshi.
Alisema mkataba wa huduma kwa mteja ni takwa la kisheria na kuwa katika uandaaji wake linatakiwa kuwa shirikishi baina ya pande zote mbili yaani kwa upande wa mamlaka(mtoa huduma) na mteja(mtumia huduma)na kuwa unaeleza wajibu wa pande zote mbili
"Tumeona ni vyema tukaanza na hawa watendaji wa kata kuwapitisha katika mkataba huu kwani ndio wasimamizi wakuu wa huduma ikiwemo maji katika ngazi za chini kabisa na itakuwa rahisi kwa wananchi kuweza kupata majibu ya maswali yao kule chini katika mitaa yao" alisema
Alisema watendaji hao wanatakiwa kuwa wa kwanza kuangalia hali ya huduma katika eneo husika na pia mkataba huu kwa sasa umefanyiwa maboresho katika baadhi ya vipengele ikiwemo mfumo wa utoaji taarifa sambamba na gharama za kuunganisha maji.
Kaimu mkurugenI wa MUWSA Edes Mushi alisema mkataba huo wa huduma kwa mteja umeweka uwazi zaidi juu ya uendeshaji wa mamlaka pamoja na wajibu baina ya pande zote mbili.
Alisema uandaaji wa mkataba huo ni shirikishi kwani jamii au watumiaji wa maji walishirikishwa kwa kutoa maoni na baada ya kuandaliwa walirudishiwa tena na kisha kuusoma na kuukubali ndipo ukapitishwa.
"Tuliwashirikisha wananchi katika hatua za awali kabisa na baada ya kupata mawazo yao tukaandaa na kisha tukarudi tena baada yao wao kuazimia ndipo ikapitishwa na mamlaka ya usimamizi wa nishati na maji(EWURA)kwani yeye ndiye msimamizi mkuu" alisema
0 Comments