Na Amon Mtega,_ Namtumbo
BAADHI ya Nyumba 130 zilizokuwa zimeezuliwa na kimbunga cha mvua katika Kijiji Cha Likuyusekamaganga Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma zimepatiwa msaada wa bati 410 kutoka katika Kampuni ya Mantra Tanzania Limited inayojishughulisha na madini aina ya Uranium katika Mto mkuju iliyopo Wilayani humo.
Akikabidhi bati hizo kwa mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dk.Julius Ningu afisa mahusiano wa kampuni ya Mantra Khadija Pallangyo amesema kampuni imetoa msaada wa bati hizo zenye thamani ya Sh.Milioni 10 kufuatia ombi la Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa la kuiomba kampuni hiyo iweze kusaidia maafa hayo.
Afisa mahusiano Pallangyo amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi na jamii hivyo ikaona ni vema kutoa msaada huo ambao baadhi yao utawasaidia kurudisha makazi yao kama awali kabla ya kupatwa na maafa hayo.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dk . Julius Ningu wakati akipokea msaada wa bati hizo ameishukuru kampuni hiyo na kuwa Serikali inaitambua kampuni hiyo kutokana na mchango wake wa mara kwa mara kwenye jamii.
Ningu amesema kuwa katika Wilaya hiyo maeneo mbalimbali ya Vijiji vya Wilaya hiyo Vilipatwa na maafa hivyo msaada utagusa katika maeneo hayo kwa kutumia utaratibu mzuri kwa kuwa baadhi ya maeneo Serikali ilishatoa msaada.
Maafa hayo yalitokea Novemba 30 mwaka 2021 katika Kijiji hicho majira ya saa 10.30 jioni mvua iliyoambatana na upepo ilinyesha kwa taklibani dakika 45 na kusabaisha Nyumba 130 kuezuliwa na mvua hiyo na kuwafanya wahanga kwenda kujisitili kwa wenzao ambao makazi yao yalisalimika.
0 Comments